WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA, DAWASA YATOA MREJESHO WA HUDUMA

Katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) imeendelea kuwafikia wateja zaidi katika mitaa mbalimbali ya Mikoa ya Dar na Pwani ili kuhakikisha wanapata huduma bora.
Akizungumza katika kipindi cha Meza ya busara kinachoruka kupitia Wapo radio, Meneja wa huduma kwa wateja DAWASA, ndugu Doreen Kiwango ameeleza kuwa wateja katika mikoa yote 23 ya kihuduma DAWASA wanaendelea kufikiwa na Mamlaka kusikilizwa, kutatua changamoto na kupokea maoni.
"Pamoja na kuwafikia nyumba kwa nyumba, tutakua na madawati ya huduma kwa wateja katika Serikali za mitaa yetu ifikapo tarehe 10 - 11/10/2024, lengo ikiwa kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaboreshea huduma, niwaahidi tu huduma kwa wateja haitaishia katika wiki hii tu bali kwetu DAWASA kazi hii ni endelevu" ameeleza ndugu Doreen.
Kwa upande wake Meneja wa Mkoa wa kihuduma DAWASA Tabata, Mhandisi Boniface Ole Philemon ameeleza kuwa lengo la Mamlaka sio kumsitishia mwananchi huduma ya maji bali kumpatia huduma hiyo kwa wakati wote.
"Tunapoendelea kupita mtaani, tupo na team ya ufundi kwajili ya kurudisha huduma kwa wananchi wanaolipia kiasi cha deni lao, lakini pia kuingia mikataba maalumu ya ulipaji wa madeni Ili mteja aweze kurudishiwa huduma na kuifurahia, tunamthamini sana mteja wetu, na kama Mamlaka mteja ndio Kipaumbele chetu kikubwa" ameeleza Mhandisi Boniface.
Wiki ya huduma kwa wateja yenye kauli mbiu isemayo " Ni zaidi ya matarajio imeanza rasmi tarehe 7/10/2024 na itafikia tamati tarehe 11/10/2024.