WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA YAADHIMISHWA KWA WANANCHI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imeendesha dawati la huduma kwa wateja kwa lengo la kuwafikia wateja wengi kwa ukaribu zaidi na kutatua changamoto mbalimbali pamoja na kukusanya maoni juu ya uboreshaji wa huduma ya maji na usafi wa mazingira.
Hatua hii, ni katika kuadhimisha Wiki ya huduma kwa wateja kwa mwaka 2025 iliyobeba kauli mbiu isemayo "Dhamira inayowezekana."
Akizungumza katika dawati hilo la huduma kwa wateja, Meneja wa Huduma kwa Wateja DAWASA, Ndugu Doreen Kiwango amesema wiki hii ni muhimu sana kwa Taasisi kwani inakumbusha uhusiano uliopo kati ya Mamlaka na wateja wake, hivyo ni muhimu kuwafikia na kuwasikiliza.
"Leo tupo hapa mtaa wa Bangulo Mwembekiboko, kata ya Pugu Station, mteja anapofika hapa tunamsikiliza changamoto na maoni yake, lakini huduma ya kuunganishiwa maji, changamoto za ankara, wateja ambao hawapati maji wote tunawahudumia katika dawati hili," amesema Kiwango.
Wananchi waliofika katika dawati hilo, wameishukuru DAWASA kwa kuwasogezea huduma karibu hasa katika kipindi hiki cha wiki ya huduma kwa wateja kwani inaonyesha kwa vitendo jinsi gani wanawajali wateja wao.
"Leo tunapata huduma tukiwa hapa mtaani kwetu, tunaipongeza DAWASA hasa tukiadhimisha wiki hii ya huduma kwa wateja, tumetatuliwa changamoto zetu kwa wepesi sana na tunaomba baada ya hapa utaratibu huu uwe wa mara kwa mara," amesema Ndugu Ally Hassan.
Dawati hili la huduma kwa wateja lilitanguliwa na watumishi wa DAWASA kupita mtaa kwa mtaa kusikiliza wananchi na kutatua changamoto zao pamoja na kupokea maoni juu ya kuboresha huduma ya maji na usafi wa mazingira.
