BENKI YA DUNIA YAIPA TANO DAWASA USIMAMIZI MIRADI
Benki ya Dunia imetembelea na kukagua utekelezaji wa Miradi inayofadhiliwa na Banki hiyo ya Usafi wa Mazingira katika Mikoa ya Dar es salaam na Pwani yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 179 na kuhimiza ukamilishaji wake kwa wakati ili kuleta tija kwa Jamii nufaika.
Katika ziara hii iliyoongozwa na mbobezi wa huduma za usambazaji Majisafi na Usafi wa Mazingira Benki ya Dunia, Bwana Ivaylo Kolev umetembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Usafi wa Mazingira inayotekelezwa Dar es Salaam kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ambayo iko hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Miradi hiyo ni pamoja na Mradi wa Usafi wa Mazingira Mbezi Beach, Mradi wa ujenzi wa mtambo wa kisasa wa kuchakata takatope Zingiziwa (Ilala), Mtamba (Kibaha), Kisopwa (Kisarawe) na Vijibweni (Kigamboni) sambamba na Mitambo ya kutibu Majitaka Sinza D na Vingunguti pamoja na Kituo cha Huduma kwa umma shekilango.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa Benki ya Dunia wameelekeza DAWASA na Wakandarasi wa Miradi kuongeza kasi katika usimamizi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kuanza kunufaisha wananchi kwa huduma bora za Usafi wa Mazingira.
Ndugu Ivaylo Kolev ametoa rai kwa DAWASA kuongeza kasi katika utekelezaji wa Miradi ili ianze kufanya kazi na kuboresha hali ya huduma ya Usafi wa Mazingira ndani ya eneo la kihuduma la DAWASA na kupunguza athari za magonjwa ya mlipuko
"Utekelezaji wa miradi hii unaridhisha lakini tunaomba wakandarasi wa miradi hii kuongeza kasi na DAWASA kusimamia kwa makini katika kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kutoa manufaa kama ilivyopangwa," amesema Ndugu Kolev.
Mkurugenzi wa Miradi na Uwekezaji DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kuwa mshirika thabiti wa maendeleo, huku akiahidi kuongeza jitihada ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ubora na kukamilika ndani ya muda uliopangwa.
