DAWASA YASHINDA TUZO UWEKEZAJI MIUNDOMBINU YA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imepata tuzo maalum ya uwekezaji katika miundombinu ya majisafi na usafi wa mazingira kwa mwaka 2026, ikiwa ni utambuzi wa jitihada zake za kupanua na kuboresha huduma hizo kwa wananchi.
Tuzo hiyo imetolewa na Chemba ya Ujenzi wa Majengo na Miundombinu Afrika Mashariki (EABC Awards) katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Everlasting Lyaro, amesema utambuzi huo unaonesha umuhimu wa uwekezaji unaofanywa na Serikali kupitia DAWASA katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira.
Amesema uwekezaji huo unahusisha ujenzi na upanuzi wa mitandao ya mabomba, matanki ya kuhifadhi maji, uboreshaji wa vituo vya uzalishaji na usambazaji wa maji pamoja na miundombinu ya majitaka.
Kwa mujibu wa Lyaro, miradi hiyo inalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji na usambazaji wa maji, kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma na kupanua wigo wa wananchi wanaofikiwa katika maeneo ya Dar es Salaam na Pwani.
Amesema tuzo hiyo itaendelea kuhamasisha DAWASA kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi kwa kuzingatia ubora, ubunifu na matumizi bora ya rasilimali, huku ikiimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya maji.
Uwekezaji katika miundombinu ya maji na majitaka unazidi kuwa muhimu kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma linalochochewa na ukuaji wa miji na idadi ya watu.
