Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
BILIONI 3.3 KUFIKISHA MAJI BANDARI KAVU YA KWALA
23 Jun, 2026
BILIONI 3.3 KUFIKISHA MAJI BANDARI KAVU YA KWALA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekamilisha maboresho ya uhuishaji wa kisima cha maji cha Kwala kilichopo kijiji cha Minazi mikinda, kwa lengo la kuwezesha uzalishaji wa maji ili kutoa huduma ya majisafi katika bandari kavu ya Kwala, iliyopo Kata ya Kwala, Kibaha vijijini, Mkoa wa Pwani.

Hayo yamesemwa na Msimamizi wa Mradi Mhandisi Ibrahim Kazumba. Amesema lengo la mradi ni kusambaza huduma ya maji katika bandari hiyo inayotarajiwa kuwa sehemu ya kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo. 

"Kwa sasa tumefanikiwa kuboresha kisima hiki kwa kukisafisha na kupima wingi wa maji na kupata matokeo mazuri yatakayosaidia kuendelea na hatua zingine," amesema Mhandisi Kazumba. 

Amesema kisima hicho kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 1.3 za maji kwa siku na kuhudumia eneo la bandari kavu, kazi itakayofanyika ni kulaza mabomba ya inchi 8 ya kupeleka huduma ya maji kutoka kwenye kisima kwenda bandari kavu kwa umbali wa kilomita 13.32. 

"Kwa sasa tunasubiri mabomba ya kusambaza maji yafike ili tuweze kujenga mtandao wa maji, tunatarajia utekelezaji wa kazi hii utaanza hivi karibuni," amesema Mhandisi Kazumba. 

Utekelezaji wa mradi huu wa kisima utagharimu Shilingi bilioni 3.3 na unatarajiwa kukidhi takribani asilimia 88 ya mahitaji ya maji ya bandari kavu ya Kwala, hatua itakayochangia kuimarisha uendeshaji wa shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.