DAWASA, VIONGOZI SARANGA WAWEKA MIKAKATI UBORESHAJI WA HUDUMA
Viongozi wa Serikali katika Kata ya Saranga kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), imefanya ziara ya kimkakati ya kukagua hali ya huduma ya maji na kukubaliana kuweka mikakati ya kuboresha huduma katika kata hiyo.
Ziara hiyo imelenga kujionea hali halisi ya upatikanaji wa huduma ya maji, kusikiliza changamoto za Wananchi pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha huduma inaimarika na kuwafikia wakazi wote.
Diwani wa Kata ya Saranga, Mhandisi John Sanga, amepongeza ushirikiano kati ya DAWASA na viongozi wa Wananchi huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua changamoto za maji kwa haraka.
“Tumetembelea mitaa katika maeneo ya Michungwani, King’ong’o na Saranga na kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji. Pia tumebaini maeneo ambayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto za muda mrefu, na sasa lengo ni kupata suluhisho litakalowezesha wananchi wote kupata huduma ya uhakika,” amesema Mhandisi Sanga.
Aidha, ameitaka DAWASA kuendelea kupanua huduma ili kuhakikisha kila eneo ndani ya kata hiyo linanufaika na huduma bora ya maji.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA,Bi Everlasting Lyaro amesema ziara hiyo imewezesha kubaini mahitaji muhimu ya wananchi na kwamba tayari Mamlaka imeanza utekelezaji wa hatua za kuboresha huduma.
Ameeleza kuwa miongoni mwa maboresho yanayoendelea ni uwekaji wa bomba la usambazaji la inchi 6 litakalounganishwa kutoka kwenye bomba kuu la inchi 48, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa kusambaza maji na kuboresha upatikanaji wa huduma katika maeneo ya Saranga na jirani zake.
Mbali na hilo, DAWASA imebainisha kuwa inaendelea na juhudi za kuongeza siku za upatikanaji wa maji, kuimarisha ushirikiano na viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na kuboresha usimamizi wa huduma ili wananchi wapate maji kwa uhakika na kwa wakati.
