CHALINZE WAKUMBUSHWA ULINZI NA UTUNZAJI WA VIZIMBA VYA MAJI

📍Bagamoyo
📌 Elimu zaidi yatolewa juu ya ulipaji wa huduma kwa njia za Wakala au Benki
📌 Wananchi watahadharishwa na vishoka, taratibu za kuunganishiwa zawekwa wazi
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa elimu ya utunzaji wa vioski (Vizimba) na miundombinu ya majisafi kwa wakazi wa vijiji vya Msinune, Rupungwi na Manga - Mkata katika Halmashauri ya Mji wa Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo.
Akiotoa elimu kwa wakazi hao, Afisa Maendeo ya jamii DAWASA, Bi Elizabeth Arajiga amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa miundombinu ya maji pamoja na vioski vya maji vinavyotoa huduma katika vijiji hivyo, ili kuendelea kupata huduma ya uhakika na kujitosheleza.
“Tusikubali kuhamasishwa na uharibifu wa miundombinu ya maji haswa hivi vioski vinavyotoa huduma katika maeneo yenu na mkibaini toeni taarifa kwa viongozi wa vijiji tuzishughulikie," alisema Arajiga.
Sambamba na ulinzi wa miundombinu, Mamlaka imehamasisha wakazi juu ya kuunganishiwa huduma ya Maji katika makazi yao na kutoa utaratibu wa kufuata ili kuunganishiwa ili kuepuka vishoka sambamba na njia za malipo kupitia njia za Mawakala au Benki na sio fedha mkononi kwa watumishi wa Mamlaka.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa kijiji cha Msinune, Ndugu Yahaya Mkweli ameishukuru DAWASA
kwa elimu iliyotolewa na kuhakikisha watasimamia miundombinu pamoja kutoa ushirikiano kwa wakati wote na kuhimiza elimu ya mara kwa mara kutolewa ili kuongeza uelewa wa huduma ya maji kwa wananchi.
"Sisi sasa tuliopata elimu hapa tukawe mabalozi kwa wenzetu tukiona uharibifu wa namna yoyote tusisite kutoa taarifa kwetu viongozi au DAWASA moja kwa moja ili hatua zaidi zichukuliwe " alisema Ndugu Mkweli.
Chalinze ni miongoni mwa maeneo ya kihuduma yanayohudumiwa na DAWASA katika Mkoa wa Pwani, maeneo mengine ni pamoja na Mkuranga, Bagamoyo, Kisarawe, Kibaha, Mlandizi, sehemu ya vijiji vya Handeni na Gwata pamoja na Ngerengere