Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA, BONDE WAMI RUVU KAZINI KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI AWESO
11 Mar, 2026
DAWASA, BONDE WAMI RUVU KAZINI KUTEKELEZA AGIZO LA WAZIRI AWESO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekamilisha zoezi la kuainisha na kutenga maeneo maalum ya uchimbaji visima virefu vya maji katika Mkoa wa Dar es salaam.

Hatua hiyo ni mojawapo ya mipango mikakati ya Mamlaka ya kuongeza uzalishaji maji chini ya ardhi kwa lengo la kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi wote. 

Akizungumza wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, Mhandisi Aziz Namanga amesema utafiti huu ulifanywa na wataalamu kutoka DAWASA wakishirikiana na Bonde la Wami Ruvu katika maeneo mbalimbali na umeleta matokeo chanya.

Baadhi ya maeneo yaliyofanyiwa tafiti ni eneo la Makuburi, Seba, Azimio na NHC (Ubungo), Makangarawe , Msufini, Dovya na Kisewe (Temeke), Luhanga na Migombani kwa Mjeshi (Ilala), Viwanja vya Benki, kwa Urassa 1, kwa Urassa 2, Kimanga, Minondo na Kichangani (Kigamboni).

Amesema zoezi hili la kuainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya uchimbaji visima ni sehemu ya utekelezaji wa Agizo la Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso (Mb) lenye lengo la kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi. 

Mhandisi Namanga amesema baada ya kuainisha maeneo hayo hatua itakayofuata itahusisha uchimbaji wa visima vya urefu wa mita 100 hadi 200 vitakavyokuwa na uwezo tofauti tofauti wa uzalishaji Maji. 

“Hii ni timu ambayo imeundwa na wataalam kutoka DAWASA na Bonde la Wami Ruvu ili kubaini maeneo bora ya uchimbaji visima ili viweze kuongeza upatikanaji wa Maji kwa Wananchi. Jumla ya maeneo tuliyobainisha ni 16  na zoezi la uchimbaji litaanza hivi karibuni” alisema Mhandisi Namanga

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Luis, Ndugu Haruna Sebarua ameishukuru Serikali kwa hatua  ya maboresho makubwa ya usimamizi wa huduma kupitia visima ambao utasadia sana kukuza upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi na kuleta unafuu. 

"Tunaishukuru Serikali na DAWASA kwa uamuzi huu na tunatamani kazi hii ianze mara moja katika maeneo yetu ili wananchi waanze kunufaika na hudum ya maji," amesema Ndugu Sebarua.