Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA, KOREA WAWEKA MIKAKATI KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI
11 Aug, 2025
DAWASA, KOREA WAWEKA MIKAKATI KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI


Ujumbe wa wabunge kutoka nchini Korea na wawakilishi wa Benki ya Exim Korea wametembelea Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na kukubaliana kuimarisha ushirikiano wa usimamizi na usambazaji wa huduma za maji.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire amesema Tanzania ina vyanzo vingi vya maji lakini changamoto iliyopo ni usimamizi na usambazaji wa rasilimali hii kwa wananchi.

"Nchi yetu haina shida ya maji, tuna vyanzo vingi vya maji kama vile mito na maziwa makubwa mfano Mto Ruvu ambao unachukua asilimia 90 ya maji yanayosambazwa katika Jiji la Dar es Salaam.

“Kupitia ujumbe huu wa nchi ya Korea, tunatarajia zaidi kuendeleza miradi ya uboreshaji huduma za maji na kukabili changamoto ya upotevu wa maji katika maeneo ya kihuduma," amesema Mhandisi Bwire.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe huo, Bi. Lee Jae Jung kwa niaba ya Korea ameridhishwa na jitihada zinazofanywa na DAWASA katika usimamizi na usambazaji wa huduma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za maji na Serikali ya Korea itaendeleza ushirikiano huu ili kuchochea na kuendelea jitihada hizo.

Ujumbe huo umefanya mazungumzo na Menejimenti ya DAWASA kuhusu fursa za kuboresha miundombinu ya huduma za maji na teknolojia za kisasa zinazoweza kuongeza ufanisi wa huduma kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Kupitia ziara hii, DAWASA na washirika hao wa kimataifa wameonesha dhamira ya kuendeleza miradi ya huduma za maji, kuboresha upatikanaji endelevu wa huduma za maji kwa wananchi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika sekta ya maji.