DAWASA YAWAPA UJUZI MWAUWASA MITA ZA MALIPO YA MAJI KABLA
Watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) wanaendelea na ziara ya mafunzo na kupata ujuzi kuhusiana matumizi ya teknolojia mpya ya matumizi ya mita za malipo kabla kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Ziara hiyo ya siku mbili imehusisha timu ya watumishi na watendaji kutoka idara na vitengo tofauti vya MWAUWASA ambao wamefika DAWASA kwa ajili ya kujifunza juu ya mita za malipo ya kabla na mafanikio mbalimbali katika sekta ya maji.
Akizungumzia mafanikio ambayo wameyapata katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa MWAUWASA, Ndugu Salustia Kusekwa ameishukuru na kuipongeza DAWASA kwa hatua waliyofikia katika matumizi ya teknolojia ya mita hizo.
"Jambo kubwa ambalo tumelipenda na kujifunza ni matumizi ya mita za malipo kabla, zinasaidia kupunguza malalamiko ya wateja, kazi yetu kubwa ni kuhudumia wananchi hivyo wakipata huduma kwa amani, nasi tunafarijika."
"Mita hizi zinampa mteja uhuru wa kupanga bajeti ya matumizi na kuondoa malimbikizo ya madeni. Ziara yetu imekuwa ya mafanikio na tija, hivyo MWAUWASA tunaahidi wateja wetu wa Mwanza tunakwenda kulianza zoezi hili kwa kasi kwasababu tumeona na kujifunza kwa vitendo," amesema Ndugu Kusekwa.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Ndugu Modesta Mushi amesema Mamlaka imefarijika kupokea ugeni toka MWAUWASA kwani kushirikishana mengi yakiwemo changamoto udhibiti wa upotevu wa maji.
"Katika majadiliano, tumetambua nasi tunapaswa kuangalia zaidi juu ya wizi wa maji na uchepushaji mabomba na kuweka utaratibu wa ufuatiliaji wa mwenendo wa matumizi ya mita za wateja mara kwa mara," amesema Ndugu Modesta.
