Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WATUMIAJI WAKUBWA WA HUDUMA ZA MAJI WAHIMIZWA KULIPA ANKARA KWA WAKATI
13 Mar, 2026
WATUMIAJI WAKUBWA WA HUDUMA ZA MAJI WAHIMIZWA KULIPA ANKARA KWA WAKATI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kupitia Mkoa wa Kihuduma Makongo imekutana na baadhi ya wateja wakubwa wa huduma za maji kwa lengo la kupokea mrejesho wa huduma na kuwahmasisha ulipaji wa ankara kwa wakati itakayosaidia uboreshaji wa huduma za Maji.

Miongoni mwa watumiaji wakubwa waliotembelewa ni pamoja na Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Ardhi, Jengo la sky city Mall, Kampuni ya Ujenzi ya China Granix pamoja na Chuo cha Takwimu.

Afisa Huduma kwa Wateja DAWASA Makongo, Ndugu Christopher Sika amesema kukutana na wateja hao  mara kwa mara ni utaratibu wa Mamlaka ya kuongeza na kuimarisha mahusiano baina ya Mamlaka na mteja kwa lengo la kutoa huduma bora na toshelevu wakati wote.

Kwa upande wake, Ndugu Zawadi Majaliwa, Mratibu wa Mali zisizohamishika (estate coordinator) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema wamefarijika kukutana na watumishi wa DAWASA ambapo imewawezesha kutoa maoni, ushauri na changamoto zao, wakiamini zitafanyiwa kazi kwa haraka na kuendelea kuboresha utoaji huduma.

Majaliwa amesema, huduma ya maji ni huduma muhimu sana hususani kwa Taasisi zinazohudumia watu wengi kwa pamoja kama vyuo hivyo kuwa karibu na DAWASA Kunaboresha sana utoaji wa huduma hiyo muhimu.