DAWASA KUBADILI TASWIRA YA USAFI BUGURUNI, WANANCHI 180,000 KUNUFAIKA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeendelea na utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa uondoshaji majitaka wa Buguruni unaolenga kuboresha hali ya usafi wa mazingira kwa wakazi wa Kata ya Buguruni, mtaa wa mivinjeni.
Mamlaka ilisanifu mradi huu kwa lengo la kuboresha huduma ya usafi wa mazingira katika eneo la Buguruni ambalo limekuwa likikabiliwa na changamoto hii kwa muda mrefu na kusababisha hatari ya magonjwa mbalimbali kwa wananchi.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huu, Msimamizi wa mradi, Mhandisi Khalid Upunda amesema utekelezaji wa mradi kwa sasa umefikia asilimia 26 na ujenzi wa miundombinu ya kupokea majitaka na kuchakata inaendelea kwa kasi katika eneo la kazi.
Pia, mradi utanufaisha wakazi wa maeneo ya Buguruni, Manispaa ya Ilala, Magomeni, Ndugumbi na Mzimuni katika Manispaa ya Kinondoni.
"Pia maeneo mengine ni Ilala Mchikichini, Kariakoo, Jangwani, Gerezani, Kisutu, Mchafukoge, Upanga Mashariki, Upanga Magharibi na Kivukoni katika Manispaa Ilala," amesema.
Mradi unatekelezwa kupitia Mhandisi kampuni ya Kolon Global Corporation chini ya Mhandisi Mshauri Kampuni ya M/s Dohwa Engineering Ltd.
"Utekelezaji wa mradi utachukua muda wa miaka mitatu, ambapo unatarajia kukamilika mwaka 2028, kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 70," amesema.
Amewataka wananchi kuwa wavumilivu na kushiriki kulinda miundombinu ya miradi ili mradi ukamilike kwa haraka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa seriali ya mtaa ya Mivinjeni, Ndugu Fadiga Mtumwa amesema mradi huu unakwenda kuwa suluhu ya matatizo mengi ya wananchi kupatwa na magonjwa ya mlipuko na magonjwa mengine.
Ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kutenga na kutekeleza mradi huu utakaoleta manufaa kwa wananchi takribani 181,440.
Naye mkazi wa mtaa wa Mivinjeni, Ndugu Ismail Ali amesema kazi hii ni kubwa na inaonekana, Serikali imefanya uamuzi sahihi wa kuwapunguzia wananchi kwa kujenga mradi huu.
