HABARI NJEMA KIBAHA! MRADI WA KISASA MAJITAKA MBIONI KUKAMILIKA
Ujenzi wa mtambo wa kisasa wa kuchakata majitaka katika eneo la Mitamba, Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, umefikia asilimia 50 ya utekelezaji wake huku lengo likiwa ni kuimarisha usafi wa mazingira kwa wananchi.
Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu, ambapo utaanza kutoa huduma muhimu za uchakataji wa majitaka na kuchangia kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira katika Wilaya ya Kibaha na maeneo ya jirani.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Msimamizi wa Mradi, Mhandisi Aden Mwaseba amesema kazi zinaendelea vizuri ambapo kwa sasa mkandarasi anaendelea na hatua ya umwagaji wa zege sambamba na ujenzi wa kuta za miundombinu mikuu ya mtambo.
“Mpaka sasa mradi umefikia asilimia 50 ya utekelezaji na kazi zinaendelea kwa kasi pamoja na kuzingatia ubora unaotakiwa. Matarajio yetu ni kuukamilisha mwezi Julai ili wananchi waanze kunufaika na huduma hii muhimu ya usafi wa mazingira,” amesema Mhandisi Mwaseba.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza uwezo wa uchakataji wa majitaka, kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuimarisha afya za wananchi, hususani maeneo yanayokuwa kwa kasi ya makazi, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Lumumba, Ndugu Amos Masamba ameipongeza DAWASA kwa kuendelea na utekelezaji wa mradi huo na kuomba ukamilike kwa wakati ili wananchi waanze kupata manufaa yaliyokusudiwa.
Amesema mtambo huo utakuwa suluhisho la kudumu katika kuboresha usafi wa mazingira na kuimarisha utoaji wa huduma za usimamizi wa majitaka.
“Mtambo huu ukikamilika utarahisisha huduma za usafi wa mazingira kwa kiasi kikubwa, kupunguza gharama za uendeshaji kwa watoa huduma na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi. Tunaamini pia utasaidia kulinda mazingira, kudhibiti uchafuzi na kuboresha afya za jamii yetu,” amesema Masamba.
Mradi huo wa kimkakati unaotekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1.8 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchakata zaidi ya lita 220,000 za majitaka kwa siku na hivyo kuboresha maisha ya wakazi wa Kibaha na maeneo ya jirani.
