Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA KUFIKISHA MAJI BANDARI KAVU YA KWALA
23 Sep, 2026
DAWASA KUFIKISHA MAJI BANDARI KAVU YA KWALA

‎Ujenzi wa mradi wa kusambaza maji katika Bandari Kavu ya Kwala, Kibaha Vijijini mkoani Pwani, umefikia hatua ya uchimbaji wa mitaro kwa ajili ya ulazaji wa mabomba ya inchi nane.

‎Msimamizi wa mradi huo, Mhandisi Ibrahim Kazumba, amesema uchimbaji wa mitaro unaendelea kwa ajili ya ulazaji wa mabomba hayo kwa urefu wa kilomita 13, ambapo hadi sasa kilomita tano zimekamilika.

‎Amesema kabla ya kuanza kazi hiyo, DAWASA ilikamilisha ukarabati, usafishaji na upimaji wa uwezo wa kisima kinachotarajiwa kuwa chanzo cha maji kwa mradi huo.

‎“Kwa sasa tunaendelea na uchimbaji wa mitaro kwa ajili ya ulazaji wa mabomba ya inchi nane kwa umbali wa kilomita 13, ambapo mpaka sasa tumefanikiwa kufikia kilomita tano,” amesema Kazumba.

‎Kwa mujibu wa Mhandisi Kazumba, amesema kisima hicho kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 1.3 za maji kwa siku, huku mradi ukitarajiwa kukidhi takribani asilimia 88 ya mahitaji ya maji ya Bandari Kavu ya Kwala.

‎Mradi huo unagharimu Sh bilioni 1.9 na unalenga kuimarisha upatikanaji wa maji katika eneo la Kwala, ambalo ni muhimu kwa shughuli za viwanda, biashara na usafirishaji.

‎Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji ya uhakika na kusaidia ufanisi wa shughuli za kiuchumi katika Bandari Kavu ya Kwala.