Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA MABWEPANDE YATETA NA WATEJA MABORESHO YA HUDUMA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA
09 Oct, 2026
DAWASA MABWEPANDE YATETA NA WATEJA MABORESHO YA HUDUMA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mabwepande imeendesha dawati la Huduma kwa Wateja katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Bunju Mkoani, Kata ya Mabwepande kwa kuwaalika wateja wa maeneo hayo kwa lengo la kupokea maoni kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi pamoja na kueleza mikakati ya kuboresha huduma katika maeneo yao. 

Uendeshaji wa Dawati hili ni sehemu ya mkakati wa Mamlaka wa kuboresha mahusiano mazuri na wateja, kusikiliza maoni na kero zao kuhusu huduma sambamba na kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja yenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kuleta tija kwa watumiaji. 

Kupitia Dawati hili, lililoratibiwa na Watumishi wa DAWASA Mabwepande, Mamlaka ilitoa nafasi kwa wananchi wa Bunju Mkoani kupata elimu na taarifa sahihi za huduma za DAWASA ikiwemo taratibu za kupata maunganisho ya majisafi, njia sahihi za kufanya malipo ya bili za maji, matumizi sahihi ya majisafi pamoja na mawasiliano rasmi ya Mamlaka. 

Pia, Mamlaka ilitoa elimu na kuwashirikisha wananchi kuhusu mkakati wa kukabiliana na upotevu wa maji katika makazi yao, pamoja na kuwasihi wananchi kuwa sehemu ya mkakati huo ili huduma ya majisafi iweze kuwa imara kila siku na bila usumbufu. 

Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2026 yameongozwa na kauli mbiu isemayo "The Extra Mile" inayoakisi utoaji wa huduma kwa viwango na ubora zaidi ili kuwafikishia wateja huduma ya majisafi ya uhakika