Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
WAKAZI 830 WA MSANGANI KUNUFAIKA NA MABORESHO YA MIUNDOMBINU YA MAJI
23 Nov, 2026
WAKAZI 830 WA MSANGANI KUNUFAIKA NA MABORESHO YA MIUNDOMBINU YA MAJI

Wakazi wapatao 830 wa maeneo ya Kiembeni, Juhudi na Madina, yaliyopo Msangani, wameanza kunufaika na huduma ya majisafi, kufuatia kukamilika kwa maboresho yaliyofanyika ya miundombinu ya usambazaji maji yaliyofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). 

Akizungumza Mhandisi wa matengenezo Ally Migeyo DAWASA Kibaha amesema maboresho hayo yamehusisha kazi ya kuboresha mfumo wa mabomba ya usambazaji maji kwa kutoa toleo kwenye bomba la inchi 30 na kuunga kwenye bomba la inchi 6, lilanoenda kulisha bomba la inchi 10, ili kuongeza ufanisi wa usambazaji maji kwa wakazi wa maeneo hayo. 

Aidha, kazi hizo zimehusisha eneo la Jeshini, ambako bomba la inchi 10 limeboreshwa kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji na kuongeza ufanisi wa mtandao wa usambazaji. 

Mamlaka imetekeleza maboresho haya, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha miundombinu ya maji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi kwa uhakika na kwa urahisi.

Kupitia maboresho hayo, wakazi wa Kiembeni, Juhudi na Madina wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji bora wa maji, kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma hiyo na kuimarisha ustawi wa maisha yao ya kila siku.

Hatua hiyo inaonesha dhamira ya DAWASA ya kuendelea kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji maji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi. 

Diwani Kata ya Msangani Mhe. Frank Msimbe amesema maboresho ya bomba kubwa la maji kwa sasa yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma, na kuondoa changamoto ya maji ya mgao katika maeneo haya.