Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA, MBUNGE, MADIWANI WAKETI KUJADILI KUBORESHA HUDUMA CHAMAZI
09 Feb, 2026
DAWASA, MBUNGE, MADIWANI WAKETI KUJADILI KUBORESHA HUDUMA CHAMAZI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekutana na Mbunge wa Jimbo la Chamazi, Mheshimiwa Abdallah Chaurembo, madiwani na  Wenyeviti wa Mitaa 22 kutoka kata za Charambe, Kilungule, Chamazi na Mianzini  kwa lengo la kutathmini hali ya huduma ya maji katika maeneo hayo na kuweka maazimio ya pamoja ya kuboresha huduma hiyo muhimu kwa wananchi.

Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Mitaa wamepata fursa ya kueleza hali ya upatikanaji wa maji ilivyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo hali ya miundombinu ya usambazaji maji, huduma kwa wateja pamoja na maoni ya uboreshaji.

Mheshimiwa Chaurembo amesema DAWASA inapaswa kuona umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa karibu na viongozi wa mitaa na wananchi katika kulinda miundombinu ya maji, kutoa taarifa kwa wakati pale kunapojitokeza hitilafu na kuhakikisha malalamiko ya wananchi yanashughulikiwa kwa haraka na ufanisi.

"Tunataka kuona utoaji wa huduma katika Jimbo la Chamazi inaimarika katika nyanja zote ikiwemo ushirikiano baina ya DAWASA na Viongozi, tayari tumeainisha maeneo yanayohitaji ufuatiliaji wa haraka, tunaamini mtaanza nayo," amesema Mheshimiwa Chaurembo

Mhandisi Damson Mponjoli, Meneja wa DAWASA Mbagala amesema Mamlaka imetenga siku 21 ili kutafuta suluhu ya uboreshaji wa Maji kwa wakazi takribani 409,728 ambao mahitaji yao yanakadiriwa kuwa Lita milioni 36.87 Kwa siku.

"Timu za ufundi wa DAWASA zitakuwa katika Jimbo la Chamazi zikitembelea mitaa yote na kubaini changamoto pamoja na kuja na suluhu na mapendekezo. Suluhu hizi zitaambatana na mipango iliyopo ya upanuzi wa mtambo wa mtoni pamoja na utekelezaji wa mradi wa Mbande -Magengeni," amesema m
Mhandisi Mponjoli

Kikao kimehitimishwa kwa kuweka maadhimio ya pamoja, yakiwemo DAWASA kuimarisha mawasiliano na viongozi wa mitaa, kufanya tathmini ya kina ya maeneo yenye upungufu mkubwa wa maji, na kuandaa ratiba ya matengenezo na upanuzi wa mtandao wa maji.