DAWASA NA JICA KUSHIRIKIANA UWEKEZAJI SEKTA YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam(DAWASA) imefanya mazungumzo na Wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) na kubainisha maeneo za mashirikiano ili kuongeza fursa za uboreshaji huduma za Maji katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire ameeleza kuwa mazungumzo hayo ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano baina ya Tanzania na Japan katika sekta ya maji, na ni hatua muhimu katika kuhakikisha huduma bora ya maji kwa wananchi.
"Ni ugeni muhimu ambao umetoa nafasi ya mazungumzo na kufungua fursa zaidi ya uwekezaji sekta ya maji Nchini husuani hapa Dar es salaam na Pwani. Tumeweka mkazo katika kuibua miradi itakayoleta tija kwa Wananchi sambamba na kupunguza upotevu wa maji" aliongeza Mhandisi Bwire
Junko Uno, Afisa wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) ambaye anahusika na usimamizi wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na miradi ya maji ameeleza kuwa wamevutiwa na jitihada za DAWASA za kuimarisha huduma na wameona uwezekano wa kuongeza ushirikiano kupitia uwekezaji kwenye Miundombinu na teknolojia rafiki kwa mazingira.
"Ni furaha kutembelea sekta ya Maji Dar na pia kutembelea miradi iliyotekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Kupitia mazungumzo haya itakuwa ni ngazi ya kudumisha ushirikiano na kuangalia maeneo kwa ajili ya uwekezaji kwa manufaa ya Wananchi na Watanzania kwa ujumla.” alifafanua