DAWASA NA KAMPENI YA USAFI, MIUNDOMBINU YA MAJITAKA YASAFISHWA KARIAKOO
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) imeunga kampeni ya kuiweka Mkoa wa Dar es salaam safi kwa kusafisha miundombinu ya majitaka katikati ya Jiji hususani maeneo Kariakoo na Posta zoezi linalofanyika usiku na mchana ikiwa pia ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kuletwa na mvua kubwa za El-Nino.
Akizungumzia zoezi hilo, Mhandisi kutoka Idara ya Usafi wq Mazingira DAWASA, Mhandisi Mubaraka Mpala ameeleza kuwa maeneo ya Posta na Kariakoo ni maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu na biashara nyingi hufanyika wakati wa mchana hivyo kuleta changamoto katika usafishaji wa miundombinu ya majitaka wakati huo sababu iliyopelekea kutekeleza kazi hiyo nyakati za usiku.
"Mamlaka inaunga mkono kampeni ya kuliweka Jiji letu safi huku ikiendelea kuchukua tahadhali dhidi ya mvua za El-Nino, usafishaji wa mara kwa mara wa miundombinu ya majitaka husaidia ufanisi na kuepusha uzibaji unaopelekea uchafuzi wa Mazingira na kuhatarisha afya za wananchi, miundombinu hii ikiwa safi italeta mazingira rafiki pia kwa wafanya biashara". Ameeleza Mhandisi Mpala
Ameongeza kuwa pamoja na zoezi hili kuendelea katika maeneo mbalimbali yenye miundombinu ya Mamlaka eneo la Kariakoo na Posta wanaliweka katika uangalizi wa karibu mara zote ili kuhakikisha wakazi na wafanyabiashara wanakua katika mazingira rafiki na hata mvua zitakaponyesha hakutatokea madhara yeyote.
Ndugu Michael William mfanyabiashara katika soko la Kariakoo ameeleza kuwa kuna matokeo chanya yamepatikana tangu kuanza kwa zoezi hilo kwani maeneo mengi yamekua safi na utiririshaji majitaka hautokei mara kwa mara.
"Hatua hii waliyoichukua DAWASA ni nzuri pamoja na ugumu wa kutekeleza kazi yao hii wakati wa mchana katika maeneo haya, tumewaona hawalali usiku wakisafisha majitaka sehemu mbalimbali, hali hii imefanya mazingira ya biashara kuboreka zaidi na kuwa masafi wakati wote katika kipindi hiki ambacho tumepewa taadhari za mvua zinazotarajiwa za El-Nino". Ameeleza ndugu Michael
