Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA NA VIONGOZI UBUNGO WAKUBALIANA KUBORESHA HUDUMA
04 Jun, 2025
DAWASA NA VIONGOZI UBUNGO WAKUBALIANA KUBORESHA HUDUMA

Wahaidi kuwa Mabalozi wa kwanza kwa wananchi juu ya huduma za Mamlaka.

Viongozi wa Serikali za Mitaa kutoka Kata za  Kibamba, Kiluvya na Kwembe Wilayani Ubungo wamepatiwa Elimu ya huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa lengo la kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumzia utekelezaji wa zoezi la utoaji elimu liloongozwa na watumishi kutoka DAWASA Kibamba, Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA - Kibamba Mhandisi Mkashida Kavishe amesema lengo la kukutana na viongozi hawa wa Serikali za Mitaa ni kufikisha elimu ya huduma zitolewazo na Mamlaka ili kuongeza ushirikiano na kuwa mabalozi wa kwanza kutoa huduma kwa wananchi.

"Elimu tunayoitoa hapa ni pamoja utunzaji wa miundombinu ya majisafi, jinsi gani mwananchi ataunganishiwa huduma ya maji kwa mara ya kwanza, elimu ya ulipaji huduma za DAWASA, pamoja na kuhamasisha wananchi waliokatiwa huduma kurudi na kurejeshewa huduma kwa makubaliano maalumu, ameeleza Mhandisi Kavishe"

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kibwegere ndugu, Humphrey Mtili amewashukuru watumishi wa DAWASA kufika ofisini na kuwapa elimu hiyo, kwani itawasaidia sana kuwaelimisha wananchi juu ya huduma za DAWASA pale wanapofika ofisi za Serikali ya Mtaa kuhitaji ufahamu wa huduma hizo.

"Ni jambo jema kutupatia elimu hii, ni dhahiri sasa nasi tutakua na majibu kwa wananchi wanaotuuliza juu ya huduma mbalimbali za DAWASA, naomba elimu hii iwe ya mara kwa mara ili DAWASA, Serikali za Mitaa pamoja na wananchi tuwe katika njia moja tunapofikisha huduma hii muhimu kwa jamii" ameeleza ndugu Mtili.

Serikali za Mitaa zilizotembelewa na kupatiwa  elimu hii kutoka DAWASA ni pamoja na Kibwegere, Hondogo, Kiluvya, Madukani, Kiluvya kwa Komba, Kiluvya Kisarawe, Malamba Mawili, King'azi B, Makurunge, Gogoni pamoja na Kibamba