DAWASA, VIONGOZI MABWEPANDE WAJADILI UBORESHAJI HUDUMA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kupitia Mkoa wa Kihuduma Mabwepande imekutana na madiwani wa kata za Mabwepande, Bunju pamoja na viongozi wa serikali za mitaa katika kikao maalum kilicholenga kufanya tathmini ya hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo hayo.
Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kukuza mahusiano na viongozi wa serikali za mitaa, kupokea maoni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha huduma ya majisafi.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa DAWASA Mabwepande, Ndugu Tumaini Mhondwa amesema Mamlaka inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuja na miradi mikubwa na midogo ya maji, uboreshaji wa miundombinu ya maji ikiwemo kufanya matengenezo ya mara kwa mara ili kuhakikisha huduma inakuwa ya uhakika zaidi kwa wananchi.
"Tunawashukuru kwa kuitikia wito na kufika katika kikao hiki, kwa ujumla hali ya upatikanaji wa maji katika eneo letu ni ya kuridhisha na kwa maeneo yenye changamoto tunaendelea na jitihada kuhakikisha huduma inaendelea kuimarika na wananchi wanafikiwa na huduma.
Tumesikia maoni yenu na tunaahidi kuyafanyia kazi, tunaomba tuendelee kushirikiana ili tufikie lengo letu la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora," amesema Ndugu Mhondwa.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Mabwepande, Mheshimiwa Adrew Mashimba amewapongeza DAWASA Mabwepande kwa kuandaa kikao hicho ambapo kimewapa fursa ya kuwasilisha maoni na mapendekezo kutoka maeneo yao ikiwemo kuharibika kwa miundombinu ya maji mara kwa mara inayosababisha upotevu wa maji na kuathiri upatikanaji wa maji.
"Tunawashukuru DAWASA kwa kuona umuhimu wa kutuita na kutupa mrejesho huu, itaturahisishia kazi yetu kwa wananchi ambapo tutakuwa na majibu.
Tunaendelea kusisitiza maeneo mengi ya huku yanaendelea kukua tuje na miradi ambayo itaenda kutatua changamoto kulingana na idadi ya watu, vilevile kuimarisha timu ya ufundi katika kupambana na mivujo na changamoto nyingine zinazokwamisha upatikanaji wa huduma," amesema Mheshimiwa Mashimba.
Aidha, kikao hicho kilitoa fursa ya kujadili maoni na kutoka na maazimio ya pamoja ya kuendeleza ushirikiano, kuimarisha mawasiliano, kuongeza ushirikiano katika ufuatiliaji wa huduma, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa miundombinu na mazingira kwa ustawi wa huduma bora.
Mkoa wa kihuduma Mabwepande unahudumia wananchi takribani 21,000 wa maeneo ya Mabwepande, Bunju B, Mji mpya, Mboko, Kihonzile, Bunju A, Bunju Mkoani, Kilungule, Dovya na Mpiji Magoe.
