DAWASA, VIONGOZI TUMBI WAAHIDI USHIRIKIANO KUBORESHA HUDUMA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) pamoja na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mawanagulani A katika Kata ya Tumbi Wilaya ya Kibaha wamekubaliana kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kwa kutoa taarifa za mara kwa mara za huduma ya Maji zitakazoleta tija katika uimarishaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa wakati Mamlaka ilipokutana na Uongozi wa Serikali ya kwa lengo la kujadili hali ya upatikanaji na usambazaji wa maji sambamba na kubaini changamoto zilizopo katika huduma ili zitatuliwe ili maji yaendelee kutiririka.
Hatua hii imetekelezwa na watumishi wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Kibaha kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na mahusiano mazuri kati ya Mamlaka na viongozi wa Serikali za Mitaa, hali itakayowezesha kubaini na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu huduma ya maji kwa wakati na hivyo kuboresha huduma kwa wananchi.
