DAWASA YAPANUA MTANDAO WA MAJI, LIPERANYA KUNUFAIKA
Moja ya mikakati ya kuhakikisha huduma ya majisafi inaendelea kuwa bora na uhakika kwa wananchi, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati mikubwa na midogo katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam na Pwani.
Kupitia utekelezaji wa miradi hiyo, mradi wa uboreshaji huduma ya majisafi Msakuzi Kwa Liperanya ni moja ya miradi midogo inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam Mkoa wa kihuduma DAWASA Ubungo unaolenga kuimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi takribani 250 wa eneo hilo.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa Miradi DAWASA Ubungo, Sheka Omari amesema utekelezaji wa mradi huo unahusisha uchimbaji pamoja na ulazaji wa mabomba ya ukubwa wa inchi 6 kwa umbali wa kilomita 2 wenye lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi 250 wa kwa Liperanya.
"Mradi huu ni mradi wa uboreshaji huduma ya majisafi ambao unahusisha uchimbaji pamoja na ulazaji wa bomba za inchi 6 kwa umbali wa kilomita 20 ila hadi sasa tayari tumechimba takribani kilomita 1.9 na kulaza mabomba, tukiwa tumebakiza hatua chache tu kukamilisha mradi huu" amesema Mhandisi Sheka
Aidha ameongeza kuwa mradi huu kukamilika kwake kutaongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wakazi 250 wa mtaa wa Liperanya na Barney iliyokuwa inapata changamoto ya huduma ya maji kwa muda mrefu.
"Utekelezaji wa mradi huu unatarajia kukamilika ifikapo Julai 10 mwaka huu, na maeneo ya Kwa Liperanya na Barney yataanza kunufaika na huduma yetu, maana haya maeneo yapo ndani ya Msakuzi yamepitiwa na utekelezaji wa mradi mkubwa wa uboreshaji huduma ya maji Msakuzi-Machimbo-Makabe kwa hiyo kupitia mradi huu maeneo haya yameweza kuwa ni moja ya maeneo nufaika" amesema Mhandisi Sheka
Kwa upande wake mkazi wa Liperanya ndugu Sauda Rashid ameipongeza DAWASA kwa kuendelea kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wateja wake pamoja na kutimiza dhamira ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani.
"Kweli niwapongeze DAWASA kwa kazi kubwa inayofanya pamoja na kutimiza ndoto na maoni ya Mhe. Rais ya kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani, na wahandisi wametueleza kuwa mpaka kufikia tarehe kumi mwezi huu wa saba mradi utakuwa umekamilika na tutaanza kutumia maji ya DAWASA" amesema ndugu Sauda.
