Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA, WAJUMBE MASHINA YA MATOSA WAJIFUNGIA KUSAKA SULUHU YA MAJI
14 Jul, 2025
DAWASA, WAJUMBE MASHINA YA MATOSA WAJIFUNGIA KUSAKA SULUHU YA MAJI

Changamoto za upatikanaji wa maji, wizi wa mita, madeni na ulinzi wa miundombinu zimewakutanisha wajumbe wa serikali ya mtaa Matosa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) ili kuzitafutia suluhu.

Uamuzi huo wa DAWASA kupitia Mkoa wa Kihuduma Makongo ni kuitikia wito wa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliyewataka kuwasikiliza wananchi juu ya kero za  maji maeneo mbalimbali na kuzitatua haraha.

Kikao hicho kimeongozwa na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Ndugu Amani Magoma na kuhudhuriwa na maafisa kutoka DAWASA pamoja na wawakilishi wa wananchi. 

Lengo kuu la kikao hiki ilikuwa ni kutoa fursa kwa wananchi kupitia wajumbe wao kueleza kero, changamoto na mapendekezo kuhusu huduma ya maji ili kuyapatia suluhisho la pamoja.

Akizungumza katika kikao hicho, Magoma amesema:"Wananchi wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu huduma ya maji, hasa maeneo ambayo hayafikiwi na mtandao wa maji, tnashukuru sana DAWASA kwa kujitokeza kuwasikiliza wananchi wetu pamoja na kuanza kutekeleza mradi wa kusogeza mtandao wa Matosa.”

Katika kikao hicho, wajumbe wameeleza kuwepo kwa maeneo kadhaa ambayo bado yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi huku wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa maji unaboreshwa kwa usawa na kwa wakati.

Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja, Ndugu Christopher Sika alisema:"Tumejipanga kuhakikisha kila mteja anapata huduma bora. Tunaendelea kuboresha mifumo yetu ya kupokea taarifa kwa wakati, lakini pia Mamlaka inaendelea na utekeleza wa mradi wa kusogeza huduma kwa wananchi eneo la Matosa, hivyo tuwaondoe shaka wananchi ambao bado hawajafikiwa na huduma.”

Masuala ya ulinzi wa miundombinu ya maji yalijitokeza pia, ambapo wananchi wamehimizwa kushirikiana na Mamlaka katika kulinda mabomba, matenki na vifaa vingine vya DAWASA ili kuhakikisha huduma inaendelea bila vikwazo.

Naye Ndugu Athumani Said, Mjumbe wa shina namba 8 eneo la kwa Mbilinyi amesema:"Changamoto nyingine kubwa ni wizi wa dira za maji unaosababisha uharibifu wa miundombinu. Tunawahimiza wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hii, kwa sababu ni mali ya umma na inatugusa sisi sote.”

Vilevile, kikao kimegusia suala la madeni ya maji, ambapo Mamlaka ilihamasisha wananchi kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati ili kuiwezesha mamlaka kuendelea kutoa huduma bora na kuwekeza zaidi katika miundombinu ya maji.

DAWASA imesisitiza kuwa itaendelea kuwa karibu na wananchi kwa kusikiliza na kutatua changamoto zinazojitokeza katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kila kaya inapata huduma ya majisafi na salama kwa maendeleo ya jamii na afya ya umma.