DAWASA WAPEWA MBINU ZA KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI NZEGA

Waaswa kuzingatia uwajibikaji, na uzalendo katika mapambano ya upotevu wa maji
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetembelea na kujifunza namna bora na mbinu za kisasa za kudhibiti upotevu wa maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Nzega (NZUWASA) ikiwa na lengo la kupunguza upotevu wa Maji na kuboresha huduma kwa Wananchi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa NZUWASA, Mhandisi Athuman Kilundumya ameeleza kuwa upotevu wa maji kwa upande wao ni asilimia 4.4, lakini mapambano ya kudhibiti upotevu wa maji yanawezekana kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa bidii kama timu katika Mamlaka za Maji.
"Maji ni Rasilimali muhimu sana, na sisi watumishi tunatakiwa kuithamini rasilimali hii na kuweka mikakati ya kudhibiti isipotee bila sababu za msingi, mapambano haya yanaanza na kila Mtumishi kuwajibika katika nafasi yake kwa kuhakikisha anadhibiti upotevu ili Wananchi waweze kupata huduma." ameeleza Mhandisi Kilundumya.
Mhandisi Kilundumya ameeleza juu ya mafanikio ya uwepo wa mita za malipo ya kabla (Pre-paid meters) na kusema kuwa NZUWASA imefanikiw kufunga Dira hizo takribani 565 kwa Wateja wa makundi tofautitofauti zikiwemo Taasisi za Ulinzi na Usalama, maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vile Shuleni pamoja vituo vya afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja DAWASA, CPA (T) Rithamary Lwabulinda ameipongeza NZUWASA kwa kuwa kinara katika mapambano ya upotevu wa Maji na kupitia ziara hiyo yatasaidia kuwajengea Watumishi ujuzi na ueledi wa namna bora ya kukabiliana na upotevu wa maji na kuisaidia Mamlaka kuokoa fedha zinazopotea.
"Nipende kumshukuru Mhandisi Kilundumya kwa kutupatia mawazo chanya ya namna ya kudhibiti kiwango cha Maji kinachopotea na ufungaji wa Mita za Malipo ya Kabla, elimu hii imetusaidia kutuwezesha kuboresha huduma tunayoitoa kwa Wananchi wa mikoa ya Dar na Pwani na itasaidia kufikia malengo tuliyojiwekea” ameeleza Lwabulinda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wenyeviti Wilaya ya Kinondoni, Ndugu Razalous Mwakiposa ameishukuru DAWASA kwa kufanikisha kuhudhuria ziara ya mafunzo na kuipongeza NZUWASA kwa hatua kubwa waliyoifikia ya kutatua changamoto ya upotevu wa maji.