DAWASA YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA, YAKUTANA NA WAKAZI KIMARA BARUTI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefungua dawati la huduma kwa wateja katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kimara Baruti, Wilaya ya Ubungo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Mteja kwa kuwasogezea wananchi huduma karibu na maeneo yao.
Dawati hilo limetoa fursa kwa wananchi wa Kimara Baruti na maeneo jirani kupata huduma na maelezo mbalimbali kuhusu masuala ya maji, ikiwemo kuwasilisha na kufuatilia kero, maombi ya maunganisho mapya, pamoja na kupata ufafanuzi kuhusu bili na huduma nyingine za DAWASA.
Kupitia dawati hilo la huduma kwa wateja, DAWASA imewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo katika kipindi hiki cha maadhimisho haya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja, huku ikisisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na Mamlaka ni muhimu katika kuboresha huduma na kuhakikisha upatikanaji wa maji unaendelea kuwa wa uhakika.
Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja 2026 imebeba kauli mbiu ya "The Extra Mile" yenye lengo la kuakisi na kuhamasisha utoaji wa huduma kwa viwango na ubora zaidi ili kuwafikishia wateja huduma ya uhakika.
