Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAANIKA MIKAKATI UIMARISHAJI WA HUDUMA YA MAJI
21 Jul, 2025
DAWASA YAANIKA MIKAKATI UIMARISHAJI WA HUDUMA YA MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeainisha mipango ya muda mfupi, ya kati na mrefu wa kuondokana na huduma ya maji ya mgao katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

Mikakati hiyo imebainishwa wakati wa ziara maalumu baina ya DAWASA na Wakuu wa Wilaya za Kinondoni (DC), Mhe. Saad Mtambule na wa Ubungo (DC), Mhe. Albert Msando ya kutembelea na kukagua miundombinu ya uzalishaji na usambazaji maji.

Katika ziara hiyo, wametembelea matenki ya kuhifadhi maji ikiwemo tanki la terminal Chuo Kikuu lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita za ujazo milioni 45, tanki la maji Tegeta A lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 5 pamoja na mtambo wa uzalishaji Maji Ruvu Chini uliopo wilayani Bagamoyo.

Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji wa Maji DAWASA, Mhandisi Leonard Msenyele amesema Mamlaka katika mwaka huu wa fedha imekwisha agiza pampu mpya sita zitakazofungwa katika mitambo ya uzalishaji maji Ruvu Juu na Ruvu Chini.

Pia, kuongeza uzalishaji wa lita milioni 90 katika mtambo wa Ruvu Chini ikiwa ni mpango wa muda mfupi katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

"Ila kwa mpango wa muda mrefu Mamlaka inatarajia kujenga mtambo wa uzalishaji Maji Rufiji ambapo ukikamilika utazalisha lita za ujazo bilioni 1.5 kwa siku," amesema Mhandisi Msenyele.

Naye Mhe. Mtambule amesema DAWASA imefanya kazi kubwa na kuleta mageuzi ya huduma ya Maji ingawa Jiji la Dar es Salaam wakazi wake wanaongezeka kwa kasi inayosababisha kuzidiwa kwa upatikanaji wa huduma ya maji kwa muda masaa 24 katika baadhi ya maeneo. 

"Ni lazima mje na mkakati mazubuti wa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji unaoakisi na ongezeko kasi la wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwa zaidi ya hata miaka kumi mbeleni," amesema Mhe. Mtambule.

Kwa upande wake, Mhe. Msando amesema katika kuboresha upatikanaji wa huduma una kwenda sambamba na kudhibiti upotevu wa maji ambapo yakiokolewa yatasaidia wananchi waliokosa huduma na kuitaka Mamlaka kuja na ubunifu wa kuzibiti mivujo kwa wakati.

"Mimi nataka niwashauri hii mivujo mafundi wenu hawawezi kuidhibiti yote kila mahali kwa wakati mmoja na huko mitaani kuna watu wana utaalum wa kuzidhiti bila nyinyi, wengine wamepita katika vyuo vya ufundi.

Nadhani mpite mitaa yote muhamasishe mpate watu kama hao ambapo mtawasajili halafu watawasaidia sana katika kukabiliana na upotevu wa maji," amesema Mhe. Msando.