Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAANZA MRADI WA MAJI SINZA A
09 Sep, 2026
DAWASA YAANZA MRADI WA MAJI SINZA A

Jumla ya wakazi 750 wa Mtaa wa Sinza kwa Remi, Kata ya Sinza A, Wilaya ya Ubungo, wanatarajiwa kunufaika na maboresho ya huduma ya maji kupitia mradi unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 20.7 unalenga kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji iliyodumu kwa muda mrefu katika maeneo ya Sinza kwa Remi, Juma Ikangaa, Sokoni, Mipango, Machungwadamu, Muungano na Hisia Kwanza, kwa kusogeza huduma ya majisafi na salama kwa wananchi.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi wa Miradi wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Magomeni, Mhandisi James Sinale, amesema mradi huo utaongeza msukumo wa maji na kusaidia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma kwa wakazi wa Sinza A na maeneo ya jirani.

Amesema kwa sasa kazi zinazoendelea ni uchimbaji na ulazaji wa mabomba yenye kipenyo cha inchi tatu kwa umbali wa mita 100 na mabomba ya inchi mbili kwa umbali wa mita 150. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sinza A, Ally Mgaya, ameipongeza DAWASA kwa kuanza kutekeleza mradi huo, akisema kasi ya kazi imewapa wananchi matumaini ya kumaliza changamoto ya maji.

Naye mkazi wa Mtaa wa Juma Ikangaa, Sharifa Kimbelembele, ameishukuru DAWASA kwa kusikia kilio cha wananchi waliokabiliwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu. Amesema mradi huo utawapunguzia wanawake adha ya kutafuta maji, akieleza kuwa “mnaenda kumtua mama ndoo ya maji kichwani.”