MIKOCHENI KUNUFAIKA NA MTANDAO MPYA WA MAJISAFI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kupitia Mkoa Kazi DAWASA Kawe, imepanga kufanya maboresho ya mtandao wa usambazaji wa maji katika mitaa ya Chwaku, Migombani na Regent, iliyopo Mikocheni, Jijini Dar es Salaam.
Maboresho hayo yanahusisha kuondoa bomba la zamani la chuma linalohudumia maeneo hayo na kuweka bomba jipya, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa mtandao wa usambazaji wa maji, kupunguza upotevu wa maji pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Mhandisi wa Mkoa Kazi DAWASA Kawe, Erasto Mwakilulele, alisema maboresho hayo yamekuja baada ya maeneo hayo kuingia katika mipaka ya Mkoa Kazi DAWASA Kawe kufuatia maboresho ya mipaka ya kiutendaji ndani ya DAWASA.
''Baada ya eneo hili kuanza kuhudumiwa na Mkoa Kazi DAWASA Kawe, Mamlaka ilipokea taarifa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu changamoto za upatikanaji wa maji. “Tumefanya tathmini na kubaini umuhimu wa kuondoa bomba la zamani la chuma linalohudumia maeneo haya na kuweka bomba jipya lenye ukubwa wa inchi 4 kwa umbali wa mita 200 ili kuboresha huduma ya maji kwa wananchi,” ameeleza Mhandisi Erasto.
Naye Rashid Abbas, mkazi na mteja wa DAWASA katika eneo hilo, amesema utekelezaji wa mpango huo wa kubadilisha bomba la zamani katika mitaa ya Chwaku na Migombani utasaidia kumaliza changamoto ya muda mrefu ya kukosekana kwa maji ya uhakika katika maeneo hayo, huku akipongeza DAWASA kwa kusikiliza na kuchukua hatua dhidi ya changamoto zinazowakabili wananchi.
