Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAANZA RASMI UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI PANGANI
20 Apr, 2025
DAWASA YAANZA RASMI UTEKELEZAJI MRADI WA MAJI PANGANI

Yakabidhi eneo la mradi kwa mkandarasi

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imemkabidhi rasmi eneo la mradi Mkandarasi Shanxi Engineering  Company kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji Pangani katika Wilaya ya Kibaha Mjini.

Tukio hilo limeshuhudiwa na viongozi wa Mkoa wa Pwani, Viongozi wa Chama na viongozi mbalimbali wa ambapo pia walipata fursa ya kutembelea maeneo yatakayotekelezwa mradi huo ikiwemo ujenzi wa tenki la lita milioni 6 pamoja na kituo cha kusukuma maji.

Akizungumza katika tukio hilo, Mbunge wa Kibaha Mjini Mhe. Silvestry Koka amesema hapo awali kata ya Pangani ilikuwa na changamoto ya upatikanaji maji hivyo kwa kuanza kwa mradi wa maji Pangani ni tumaini kwa maendeleo ya Kibaha mjini.

"Katika Wilaya ya Kibaha mjini ni kata ya Pangani ndio ilikuwa ikitukwamisha kufikia asilimia 100 ya utekelezaji wa ilani ya CCM, leo tunafarijika kuona utekelezaji umeanza."amesema 

Mheshimiwa Koka ametoa rai kwa watekelezaji na wasimamizi wa mradi kukamilisha mradi kwa wakati huku pia wakiweka miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi wakati shughuli nyingine zikiendelea.

Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Ramadhani Mtindasi amesema utekelezaji wa mradi huo wenye thamani ya tsh bilioni 9.8 unaanza mara moja na utatumia muda wa miezi 12 kukamilika kwake.

"Tayari mkandarasi yuko katika eneo la mradi akiendelea na kazi, tunategemea mradi huu utatekelezwa ndani ya miezi 12 na kuanza kunufaisha wakazi takribani 80,000 wa maeneo ya Pangani, Kibaha - Msufini, Lulanzi na TAMCO. " ameeleza

Mradi wa Maji Pangani unajumuisha ujenzi wa tenki la lita milioni 6, ujenzi wa kituo cha kusukuma maji pamoja na ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha maji na usambazaji maji kwa umbali wa kilomita 18.7.