DAWASA YABORESHA KISIMA KEKO BORA KUIMARISHA HUDUMA YA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekamilisha zoezi la kufufua na kuboresha kisima cha kuzalisha maji cha Keko Bora kilichopo Mtaa wa Bora, Kata ya Chang’ombe, Wilaya ya Temeke, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa kazi hiyo, Kaimu Meneja wa Huduma za Visima wa DAWASA, Mhandisi Francisca Merere, amesema kukamilika kwa zoezi hilo ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika.
Amesema timu ya wataalamu wa mamlaka hiyo ilifanya kazi kwa ufanisi mkubwa kufanikisha ukarabati na kurejesha kisima hicho katika uzalishaji.
“Pampu mpya imefungwa na kisima kimeanza kuzalisha takribani lita 120,000 za maji kwa siku. Aidha, kisima hiki tayari kimeunganishwa kwenye mfumo uliopo wa usambazaji maji, hali itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwa wateja wa maeneo ya jirani,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa wakazi wa Mtaa wa Bora pamoja na maeneo ya karibu tayari wameanza kunufaika na huduma hiyo muhimu ya maji safi na salama.
Kwa upande wake, DAWASA imeeleza kuwa itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali na kufanya maboresho ya miundombinu ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, endelevu na yenye uhakika.
