Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YACHIMBA KISIMA MAKUBURI KIBANGU KUBORESHA HUDUMA YA MAJI KWA WANANCHI
16 Nov, 2026
DAWASA YACHIMBA KISIMA MAKUBURI KIBANGU KUBORESHA HUDUMA YA MAJI KWA WANANCHI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inatekeleza mradi wa uchimbaji wa kisima cha maji katika eneo la Makuburi Kibangu, kwa lengo la kuimarisha  upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi wapatao 1152.

Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi milioni 168 unahusisha uchimbaji wa kisima, ufungaji wa pampu ya maji, ujenzi wa nyumba ya pampu (Pump House), pamoja na ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji kutoka kwenye kisima hadi kwenye tanki la Makuburi Kibangu kwa ajili ya kurahisisha usambazaji wa maji kwa wananchi.

Akizungumza msimamizi wa Mradi kutoka DAWASA Mhandisi Aziz Namanga amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Makuburi Kibangu, ambapo utaenda kuongeza msukumo wa maji na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa majisafi kwa wakazi wa mtaa wa Mkombozi, Makuburi na Kibangu Kata ya Makuburi.

"Hadi sasa tumefikia asilimia 15 za utekelezaji, kisima kimeshachimbwa na leo tumesafisha na kuchukua sampuli ya kupima ubora wa maji kwa ajili ya hatua inayofuata ya ufungaji wa pampu na ukarabati wa nyumba ya pampu pamoja na tenki na tunategemea mradi utakamilika mwishoni mwa mwezi disemba" amesema Mhandisi Namanga

Naye, Diwani wa Kata ya Makuburi Mheshimiwa Issa Ahmed Faru ameipongeza Mamlaka kwa kutekeleza mradi huu kwa kasi ambao utaenda kumaliza changamoto ya msukumo mdogo na upatikanaji wa maji kwa mgao kwa baadhi ya maeneo.

"Tupo hapa leo ni siku ya tatu usiku na mchana na timu ya wataalamu kutoka DAWASA ipo hapa inaendelea na kazi, Mradi huu ni wa muhimu sana kwa wakazi wa Makuburi sasa tunasubiri ukamilike na wananchi wapate huduma" amesema Mheshimiwa Faru

Mamlaka inaendelea kutekeleza miradi ya kuboresha na kupanua miundombinu ya majisafi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji iliyo endelevu na ya uhakika.