KAMPENI YA USAFI DAR: DAWASA YAWEKA WAZI MWELEKEO WAKE
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imesema inaendelea kutekeleza miradi ya usafi wa mazingira yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 200, ikiwamo ya Mbezi Beach na Buguruni, ili kuboresha uondoshaji na uchakataji wa majitaka jijini Dar es Salaam.
Miradi hiyo imetajwa na Meneja DAWASA Kinondoni, Victoria Masele, aliyekuwa akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka hiyo katika uzinduzi wa Kampeni ya Usafi wa Mazingira na ugawaji wa vifaa vya usafi Mkoa wa Dar es Salaam, uliofanyika katika viwanja vya Posta, Kijitonyama.
Masele amesema DAWASA inaunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha usafi wa mazingira kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya majitaka pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira.
Amesema miradi ya kuchakata na kutibu majitaka ya Mbezi Beach na ule wa usafi wa mazingira katika Jiji la Dar es Salaam unaotekelezwa Buguruni inalenga kuboresha huduma hizo na kupunguza hatari ya magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.
Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka viongozi wa taasisi za umma kushirikiana na ofisi yake pamoja na wakuu wa wilaya kuhakikisha maeneo yote yanakuwa safi na kanuni za usafi zinazingatiwa.
Chalamila amesema jukumu la kudumisha usafi wa mazingira linapaswa kuwa la kila mmoja, bila kujali itikadi za kisiasa, dini au umri, akihimiza ushirikiano kuanzia ngazi ya mtaa hadi mkoa.
Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha uwajibikaji wa pamoja katika kudumisha usafi wa mazingira na kukabiliana na changamoto zinazoweza kuchochewa na mvua.
