Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAIMARISHA USAFI SHULE YA UHURU MCHANGANYIKO
16 Oct, 2026
DAWASA YAIMARISHA USAFI SHULE YA UHURU MCHANGANYIKO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekabidhi vifaa vya usafi wa mazingira kwa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko iliyopo Kariakoo, Wilaya ya Ilala, huku wanafunzi wakipatiwa elimu ya kutunza mazingira na kulinda miundombinu ya maji na usafi wa mazingira kuelekea kipindi cha mvua za El Nino.

Hatua hiyo inalenga kuhamasisha wanafunzi kuzingatia usafi wa vyoo na maeneo ya shule, pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya mafuriko na magonjwa yanayoweza kusababishwa na uchafuzi wa mazingira.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Afisa Maendeleo kwa Jamii wa DAWASA Ndugu Vivian Temu, amesema usafi wa mazingira ni muhimu katika kulinda afya za wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Amewahimiza wanafunzi kuwa mabalozi wa usafi kwa kuzingatia kanuni za usafi shuleni, nyumbani na katika maeneo wanayoishi.

“Tumeona umuhimu wa kuwakumbusha wanafunzi kuhusu utunzaji wa mazingira, hasa usafi wa vyoo, kuelekea kipindi cha mvua za El Nino ili kupunguza hatari ya mafuriko na kuenea kwa magonjwa. Pia tumewaletea vifaa vya usafi vitakavyorahisisha utekelezaji wa shughuli hizo,” amesema Temu.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Ajirath Kashakara, ameishukuru DAWASA kwa kutoa vifaa hivyo na elimu kuhusu matumizi sahihi ya maji na namna ya kulinda miundombinu ya majisafi na usafi wa mazingira.

Amesema ushirikiano huo utasaidia shule kuimarisha usafi, hususan wa vyoo, na kuwajengea wanafunzi uelewa wa umuhimu wa kutunza mazingira na kuzuia uchafuzi.

“Tunaishukuru DAWASA kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za elimu katika kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa usafi wa mazingira. Vifaa hivi vitasaidia shule kudumisha usafi, hasa wa vyoo, ambao ni muhimu kwa afya za wanafunzi,” amesema Kashakara.

DAWASA inaeleza kuwa kutoa elimu kwa wanafunzi ni sehemu ya juhudi za kujenga kizazi chenye uelewa na uwajibikaji katika usafi na utunzaji wa mazingira, pamoja na kulinda miundombinu ya maji na usafi wa mazingira.