DAWASA YAWEKA KAMBI KILUVYA NA KISARAWE KUDHIBITI UPOTEVU WA MAJI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kupitia Mkoa wa Kihuduma Kisarawe, imeweka kambi katika maeneo ya Kata za Kiluvya na Kisarawe kwa ajili ya kuendesha operesheni ya kubaini na kurekebisha mivujo ya maji ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza upotevu wa maji na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wateja.
Operesheni hiyo inahusisha maeneo mbalimbali ikiwemo mitaa ya Sanze, Matumbini, Vigungu, Vibula, Vigama, Kimani, Ngugu, Dunda na Bamita katika Kata ya Kisarawe, pamoja na maeneo ya Kisopwa, Kiluvya Madukani, NSSF, Makurunge, Santiago, Kwa Urassa, Kwa Komba, Fourty Lounge, Redomax na Kwa Mtenga katika Kata ya Kiluvya.
Katika operesheni hiyo, mafundi wa DAWASA wanaendelea kukagua mtandao wa usambazaji, kubaini na kuziba mivujo, kutengeneza mabomba yaliyopasuka na kurekebisha uvujaji katika mita za maji pamoja na maungio ya mabomba ili kuzuia maji kupotea kabla hayajawafikia wateja.
Matengenezo hayo yanahusisha mabomba yenye vipenyo vya inchi 1, 2, 3, 4 na 6 ikiwa ni hatua inayolenga kupunguza upotevu wa maji katika miundombinu ya usambazaji na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wateja katika maeneo husika.
Jitihada hizo ni sehemu ya mkakati wa DAWASA wa kudhibiti maji yasiyoingiza mapato (Non-Revenue Water – NRW) kwa kupunguza upotevu unaotokana na mivujo na kuimarisha matumizi bora ya rasilimali za maji, ili maji yanayozalishwa yawafikie wateja kwa ufanisi zaidi.
DAWASA inawahimiza wananchi wa Kata za Kiluvya na Kisarawe kuendelea kutoa taarifa za mivujo ya mabomba, mita zinazovuja na matumizi yasiyo halali ya huduma ya maji kupitia namba ya huduma kwa wateja 181, inayopatikana bila malipo, ili kuwezesha hatua za kiufundi kuchukuliwa kwa wakati na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji.
