DAWASA YAIMARISHA USAFI WA MAZINGIRA KUPITIA MRADI WA MAJITAKA MWENGE
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) inaendelea kuboresha miundombinu ya majitaka eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam kwa kutekeleza mradi wa usafi wa mazingira Mwenge, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Mamlaka kuimarisha usafi wa mazingira katika eneo lake la kihuduma.
Msimamizi wa miundombinu ya majitaka wa DAWASA, Mhandisi Mubaraka Mpala, amesema maboresho hayo yanalenga kuongeza uwezo wa mfumo wa majitaka, kupunguza kufurika kwa majitaka na kulinda afya za wananchi pamoja na mazingira.
Ameeleza kuwa kazi hiyo inahusisha kubadilisha mabomba ya zamani na kuweka mabomba yenye uwezo mkubwa zaidi, yakiwemo bomba la kipenyo cha inchi 16 kwa urefu wa mita 540 na bomba la inchi 10 kwa urefu wa mita 440.
"Maboresho hayo yanatarajiwa kunufaisha zaidi ya kaya 500 katika maeneo ya Mlimani City, Mwege, Mawasiliano na Sinza, kwa kuwahakikishia wakazi usafi na usala wa mazingira yao ya kila siku na kuwaepusha na magonjwa yanayoweza kutokana na uchafuzi wa mazingira kama vile kipindupindu" ameeleza Mhandisi Mbaraka.
Kwa upande wake, Mkazi wa Mwenge, Walter Mushi, ameipongeza DAWASA kwa hatua hiyo na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza maboresho katika maeneo mengine yenye mtandao wa majitaka ili wananchi waweze kufanya shughuli zao za kila siku katika mazingira masafi na rafiki.
DAWASA inawahimiza wananchi kutupa taka katika maeneo yaliyotengwa na kuepuka kuzitupa kwenye mitaro na mifumo ya majitaka ili kuzuia vizuizi na kufurika kwa majitaka. Kazi ya utekelezaji wa mradi huu wa usafi wa mazingira Mwenge inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 31, 2026, kwa lengo la kuimarisha huduma na kuongeza utayari wa miundombinu wakati wa mvua kubwa.
