DAWASA YAJIPANGA KUTUMIA MAJI YA BAHARI KUBORESHA HUDUMA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetangaza mpango wa muda mrefu wa kutumia maji ya bahari kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kukabili changamoto ya upungufu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam
Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Ndele Mengo, wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha Watendaji wa DAWASA, Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo, pamoja na wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa wilaya hiyo
Mhandisi Mengo ameeleza kuwa katika mipango ya muda mrefu, DAWASA inalenga kuwashirikisha wawekezaji binafsi wenye nia na teknolojia ya kuchuja na kusafisha maji ya bahari na kisha kuiuzia DAWASA ili itawanyie wananchi maji hayo
Mbali na mpango wa maji ya bahari, Mhandisi Mengo amebainisha kuwa DAWASA pia ipo katika hatua za mwisho za upembuzi yakinifu wa mradi mwingine mkubwa wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji ambao mshauri elekezi ameshakamilisha takribani asilimia 90 ya kazi, utatekelezwa kwa awamu nne, ambapo awamu ya kwanza pekee itazalisha lita milioni 375 kwa siku na kuondoa karibu upungufu wote wa sasa.
