Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAKABIDHI ENEO LA UJENZI WA TENKI MSUMI
09 Mar, 2026
DAWASA YAKABIDHI ENEO LA UJENZI WA TENKI MSUMI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekabidhi rasmi eneo la ujenzi wa tenki la maji litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi lita 500,000 katika eneo la Mbezi Msumi kwa mkandarasi Jeccs Construction and Supply Limted.

Hatua hiyo ni kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za ujenzi ambao unakwenda sambamba na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kilichofika asilimia 75 ya utekelezaji wake.

Akizungumza wakati wa zoezi ya makabidhiano ya eneo hilo, Kaimu Meneja wa DAWASA Ubungo, Mhandisi Alphonce Magoma  amesema kazi ya ujenzi wa tenki hilo ni miezi sita na litakapokamilika litahudumia wakazi 47,000 wa maeneo ya Msumi A, Msumi B, Msumi C na maeneo jirani.

"Kazi ya ujenzi itaanza tarehe 9.3.2026 na inakwenda sambamba na ujenzi wa kituo cha kusukuma maji kilichofika asilimia 75, tunashukuru viongozi wa Serikali kwa kuendelea kushirikiana nasi ambapo sasa tunaendelea kupokea maombi ya maunganisho mapya," amesema Mhandisi Magoma.

Mhandisi Frank Manyila, mkandarasi Jeccs Construction ameahidi kutekeleza mradi huo kwa kuzingatia viwango vya ubora, kuzingatia muda uliopangwa pamoja na masharti yote ya mkataba ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa mafanikio.

"Tumepokea eneo la ujenzi wa Tenki kutoka kwa DAWASA, kutokana na uzoefu wetu tuna ahidi kufanya kazi kwa kuzingatia ubora na muda uliopangwa ili kuboresha huduma kwa wakazi wa Msumi," amesema Mhandisi Manyila.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Msumi, Ndugu Jacqueline Juma ameishukuru DAWASA kwa kuendelea kutekeleza ilani ya Serikali inayolenga kumtua mama ndoo kichwani na kuahidi kushirikiana na DAWASA wakati wote wa ujenzi na ukamilishwaji wa mradi huo.

Ujenzi wa tenki hilo utasaidia kuongeza uwezo wa kuhifadhi maji, kuboresha usambazaji na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika zaidi.