Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAPIGA HATUA MWENGE, MRADI WA MAJITAKA WAFIKIA ASILIMIA 60
18 Nov, 2026
DAWASA YAPIGA HATUA MWENGE, MRADI WA MAJITAKA WAFIKIA ASILIMIA 60

Mradi wa uboreshaaji usafi wa mazingira eneo la Mwenge unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) kwa gharama za shilingi Milioni 600 umefikia asilimia 60 ya utekelezaji wake huku kazi ya uchimbaji na ulazaji wa bomba zenye ukubwa wa inchi 16 kwa umbali wa mita 540 na inchi 10 kwa umbali wa mita 440 zikienda kwa kasi inayoridhisha.

Akiongelea maendeleo ya utekelezaji wa kazi hiyo, Meneja idara ya Usafi wa Mazingira Mhandisi Jolyce Mwanjee ameeleza kua wamekua wakifanya kazi hiyo usiku na mchana ili kuhakikisha inakamilika na wananchi wananufaika nayo.

"Hadi sasa Kazi ipo asilimia 60 ya utekelezaji, tunaendelea na kubadilisha bomba la zamani la zege ambalo ufanisi wake ulipungua na kuweka bomba jipya la Plastiki (PVC) ili tuweze kuboresha hali ya uondoshaji majitaka katika eneo la Mwenge" ameeleza Mhandisi Mwanjee.

Mwanjee ameongeza kuwa kukamilika kwa kazi hii kutaboresha usafi wa mazingira kwa kaya zaidi ya 500 katika maeneo ya Mwenge, Mlimani City, Mawasiliano hadi Sinza na kutamaliza changamoto ya majitaka iliyopelekea uchafuzi wa mazingira na kuhatarisha jamii na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Ndugu Philipo Mwenda mkazi wa Mwenge ameeleza kuwa wanathamini jitihada zinazofanywa na DAWASA na kuwaomba kuongeza kazi ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

"Tunawashukuru kwa kazi hii ya kutuboreshea mazingira, hii itatusaidia kuwa na mazingira safi na  salama majumbani lakini hata sehemu zetu za biashara, tunaona kazi kubwa wanayofanya kila siku, tunawaomba DAWASA kuendelea kupambana kumaliza kwa wakati na ikiwezekana kuwahi kipindi cha mvua ambacho adha ya utiririshaji majitaka huwa kubwa zaidi" ameeleza ndugu Mwenda.