MIKAKATI KUBORESHA HUDUMA CHALINZE, DAWASA YATETA NA MADIWANI
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeshiriki katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Chalinze, wilayani Bagamoyo na kubainisha mikakati ya kuboresha upatikanaji wa huduma ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kimkakati pamoja na uimarishaji wa miundombinu ya muda mrefu.
Akizungumza wakati wa kikao, Meneja wa DAWASA Chalinze, Mhandisi Boniface Ole Philemon ameeleza dhamira ya Mamlaka ya kuendelea kushirikiana na viongozi hususani Waheshimiwa Madiwani ili kuhakikisha maeneo ambayo bado yanachangamoto ya huduma wanafikiwa na kupatiwa ufumbuzi.
"Tumepata fursa ya kushiriki katika kikao muhimu cha baraza la madiwani lengo likiwa ni kubainisha mikakati yetu ya kuimarisha huduma lakini kama wadau muhimu tumeomba ushirikiano wao ili kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi kwa uhakika na kwa wakati" amesema Mhandisi Boniface
Naye Mwenyekiti wa halmadhauri ya mji wa Chalinze, Mheshimiwa Leon Lucas Mgweno ameipongeza DAWASA kwa kuwa taasisi ya mfano inayoshirikiana na viongozi katika kuleta mageuzi ya utoaji huduma kwa wananchi wa Chalinze.
"DAWASA wameshiriki katika kikao rasmi cha baraza la Madiwani wa Halmashauri yetu ya Chalinze na wamepata fursa ya kueleza changamoto zilizopo na mipango waliyonayo kukabiliana hizo, pia madiwani wamepata fursa ya kuuliza maswali ya huduma ya maji na DAWASA wametoa majibu yenye ufafanuzi wa tija" amesema Mhe. Mgweno
