Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YASISITIZA WANANCHI KUWA NA VYOMBO VYA KUHIFADHI MAJI
29 Oct, 2026
DAWASA YASISITIZA WANANCHI KUWA NA VYOMBO VYA KUHIFADHI MAJI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekabidhi tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 2,000 katika Ofisi ya Kata ya Saranga, Mtaa wa Matangini, Wilaya ya Ubungo, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kuwa na vyombo vya kuhifadhi maji ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo pindi inapotokea.

Hatua hiyo inalenga kusisitiza umuhimu wa kuhifadhi maji wakati huduma inapopatikana ili yaweze kutumika wakati kutakapotokea changammoto ya kihuduma jambo litakalowapunguzia usumbufu katika shughuli za kila siku.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Meneja wa DAWASA Ubungo, Mhandisi Anthony Budaga, aliyemwakilisha Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa mamlaka hiyo  Everlasting Lyaro, amesema tanki hilo litasaidia ofisi ya kata kuwa na akiba ya maji na ni mfano wa umuhimu wa kuwa na vyombo vya kuhifadhia maji.

“Tanki hili litasaidia kuhifadhi maji katika ofisi hii ya kata. Awali, walikuwa wakichota maji moja kwa moja kutoka kwenye bomba, hivyo huduma ilipokatika, ofisi ilikosa maji na watumishi kupata usumbufu. Kupitia tanki hili, maji yataweza kuhifadhiwa kwa matumizi wakati huduma inapokosekana,” amesema Budaga.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kujenga utamaduni wa kuhifadhi maji katika vyombo vinavyofaa wakati huduma inapopatikana, ili kuwa na akiba ya kutumia pindi changamoto za usambazaji zinapotokea.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Saranga, John Jeremiah Sanga, ameishukuru DAWASA kwa kutoa tanki hilo, akisema litasaidia kupunguza changamoto ya maji katika ofisi ya kata, ambayo imekuwa ikikabiliwa na usumbufu hasa wakati wa mgao wa maji.

Sanga amesema awali, watumishi walilazimika kwenda maeneo mengine kutafuta maji huduma ilipokatika, hivyo uwepo wa tanki hilo utasaidia kuboresha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya ofisi. Pia ameeleza matumaini kuwa hatua hiyo itaongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi maji.

DAWASA inaendelea kuhimiza matumizi sahihi ya maji na umuhimu wa kuwa na vyombo vya kuhifadhia maji, ili kaya, taasisi na maeneo ya kazi yaweze kuwa na akiba ya kutumia wakati huduma inapopata changamoto. Ujumbe huo unalenga kuimarisha maandalizi ya wananchi na kupunguza athari za kukosekana kwa maji katika shughuli za kila siku.