Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YATAKIWA KUBORESHA UPATIKANAJI MAJI SEGEREA
28 Nov, 2026
DAWASA YATAKIWA KUBORESHA UPATIKANAJI MAJI SEGEREA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imepewa siku saba kuanzia Novemba 27, mwaka huu, kutafuta suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa maji katika eneo la Segerea, jijini Dar es Salaam.

Aidha, mamlaka imetakiwa kuhakikisha ratiba za upatikaji wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam zinaendana na hali halisi ya upatikanaji wa huduma na kuzingatia muda unaofaa kwa wateja.

Maagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, katika kikao kazi na menejimenti ya DAWASA, ambapo ameitaka mamlaka hiyo kufanya marekebisho ya kiufundi yatakayoongeza mgandamizo wa maji ili maeneo yenye miinuko nayo yapate huduma.

Amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia za kisasa kudhibiti maji yasiyolipiwa (NRW), ikiwamo kuzuia uingiliaji wa miundombinu ya maji na vitendo vinavyochangia upotevu wa rasilimali hiyo.

Aidha, ameitaka DAWASA kuendeleza zoezi la kufunga mita kubwa za kupima kiasi cha maji kinachoelekezwa kwa wateja katika maeneo ya huduma ya kila mkoa, ili kuboresha usimamizi wa usambazaji na kudhibiti upotevu.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri ameitaka DAWASA kutekeleza agizo la Rais Dk. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha wateja hawatozwi ankara zisizo sahihi, maarufu kama ankara za kubambikiziwa.

Kikao kazi hicho kimewashirikisha Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Bakari Shingo, na Mbunge wa Jimbo la Segerea, Agnesta Lambert Kaiza.