Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YATEKELEZA AGIZO LA DC MPOGOLO KIMANGA
10 Sep, 2026
DAWASA YATEKELEZA AGIZO LA DC MPOGOLO KIMANGA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza kutekeleza agizo la Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, la kurejesha huduma ya maji kwa wananchi wa Kata ya Kimanga, hususan Mtaa wa Darajani, ndani ya muda uliowekwa.

‎Meneja wa DAWASA Tabata, Gilbert Masawe, amesema kazi za Mradi wa Maji Tabata-Kimanga zimefikia asilimia 50 na mamlaka inalenga kukamilisha ndani ya siku 14, ikiwa ni muda mfupi kuliko siku 21 ilizopewa na Mkuu wa Wilaya.

‎Amesema mradi huo unahusisha ulazaji wa bomba la inchi nane kwa urefu wa kilomita 1.7 kutoka Kisima cha Kisiwani hadi Tenki la Masoko, ufungaji wa pampu katika Kisima cha Tabata Kisiwani pamoja na ukarabati wa Tenki la Masoko.

‎“Tangu tumepokea maelekezo, leo ni siku ya nane tupo site kuhakikisha mradi unakamilika na wananchi waanze kupata huduma. Kwa kasi iliyopo, tunatarajia kukamilisha ndani ya siku 14,” amesema Masawe.

‎Mwenyekiti wa Mtaa wa Darajani, Marius Ally, amesema wananchi wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa maji kwa muda mrefu, hali iliyowalazimu kutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo kwa ajili ya mahitaji ya kila siku.

‎Ally amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kusikiliza kilio cha wananchi na kuielekeza DAWASA kuchukua hatua, akisema maendeleo ya mradi yamewapa matumaini kuwa changamoto hiyo itamalizika hivi karibuni.

‎Mradi wa Tabata-Kimanga unagharimu Sh milioni 269 kutoka fedha za ndani za DAWASA na unatarajiwa kunufaisha takribani kaya 3,132 katika maeneo ya Darajani, Twiga na Kisiwani, Kata ya Kimanga.