Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YATOA SULUHU YA KUDUMU MBEZI
02 Feb, 2026
DAWASA YATOA SULUHU YA KUDUMU MBEZI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imewahakikishia Wakazi wa Kata ya Mbezi katika Wilaya ya Ubungo Mkoani Dar es salaam kuwa imejipanga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika kata hiyo.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa kikao kazi cha kupokea changamoto za kihuduma kilichofanywa na Mamlaka pamoja na Wakazi wa kata ya Mbezi na kilicholenga kukubaliana kushirikiana kutatua changamoto zilizopo.

Kaimu Meneja wa DAWASA Ubungo Mhandisi Alphonce Magoma ameeleza kuwa Mamlaka imejipanga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi kwa kutoa katika mfumo wa bomba kubwa eneo la Spencon na kuongeza muda wa usambazaji kutoka siku 2 hadi siku 4 kwa wiki ilikuwezesha kuwafikia wananchi wengi na muda mrefu.

"DAWASA  tumeadhimia kuwa katika mgao wa Maji katika Kata ya mbezi kuanzia siku ya Alhamisi, Februari 4,2026  tutapita katika mitaa yenye changamoto ambayo ni Mbezi Luis, Makabe na Luis ili kuhakikisha tunamaliza changamoto pamoja kutoa msaada wa kiufundi" alisema Magoma

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mbezi Mhe. Pius Ragero amepongeza DAWASA kwa kuitikia wito wa haraka na kushiriki katika kikao hicho cha wananchi ambapo kimeongeza uelewa wa mikakati iliyopo katika kuboresha upatikanaji wa maji katika maeneo yenye changamoto ya muda mrefu.

“Kama wawakilishi wa Wananchi tulipokea malalamiko yao juu ya huduma hafifu ya Maji katika baadhi ya mitaa katika kata yetu, na leo asubuh tuliwaita DAWASA ili watueleze kwa kina juu ya mipango ya kukwamua shida hii ili kuleta uelewa wa pamoja” alisema Mhe Ragero

Naye Mwenyekiti wa mtaa Mbezi Luis, Ndugu Bawaziri Hassan ameeleza kuwa huduma ya maji ni muhimu hivyo Mamlaka ihakikishe mikakati iliyotolewa inatekelezwa na iwe endelevu.