Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YATOA UHAKIKA WA MAJI MSUMI FEBRUARI HII
07 Feb, 2026
DAWASA YATOA UHAKIKA WA MAJI MSUMI FEBRUARI HII

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)imewahakikishia wakazi wa mtaa wa Msumi, Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi huu huduma ya majisafi itapatikana kikamilifu. 

Tamko hili linakuja kufuatia kukamilika kwa mradi unaotekelezwa eneo hilo unaotarajiwa kunufaisha wakazi takribani 47,000 wa mtaa wa Msumi A, Msumi B, Msumi C pamoja na maeneo jirani.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, msimamizi wa mradi, Mhandisi Azizi Namanga amesema hadi sasa kazi ya ulazaji bomba kwa umbali wa kilomita 14 imekamilika, na kazi kubwa inayoendelea ni ya ujenzi wa kituo cha kusukuma maji huku hatua nyingine ya mradi ikihusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji la lita 500,000.

"Baada ya kupokea fedha alizoahidi Mheshimiwa Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (Mb)kiasi cha Shilingi Milioni 500, kazi ya ujenzi wa kituo cha kusukuma maji imeanza mara moja ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji, ni mategemeo yetu ifikapo Februari 22, 2026 tutakamilisha kazi hii na kusukuma maji kwenda kwa wananchi," amesema Mhandisi Namanga.

Mwenyekiti wa mtaa wa Msumi, Ndugu Jacqueline Juma amesema hali ya upatikanaji wa maji mtaani hapo ilikuwa sio ya kuridhisha na wananchi wengi waliingia gharama kubwa kupata huduma ya maji, lakini juhudi zinazofanywa na Serikali kupitia DAWASA mtaani hapo zinawapa imani juu ya upatikanaji wa majisafi na salama.

"Tumekuwa tukinunua maji chumvi kwa wenye visima kwa kuuziwa kwa unit 1 kwa bei hadi ya Shilingi 4,000 hii ni gharama kubwa sana, tunashukuru Serikali ilileta fedha za kutekeleza mradi wa maji Msumi zaidi ya Shilingi Bilioni 2 na mradi unakwenda kwa kasi inayoridhisha," amesema Ndugu Jacqueline.

Ndugu Yahaya Iddy, Mkazi wa mtaa wa Msumi amesema kukamilika kwa mradi kutawapunguzia gharama za maisha kwa kupata maji kwa bei nafuu, lakini zaidi kutaboresha afya zao kwani watakuwa na uhakika wa maji wanayoyatumia ni safi na salama., na kuiomba DAWASA kukamilisha mradi huu ndani ya muda mfupi ili wananchi wa Msumi waanze kunufaika na huduma ya maji.