DAWASA YATOA WITO MATUMIZI SAHIHI MIUNDOMBINU MAJITAKA KIPINDI CHA MVUA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetoa wito kwa wananchi kutumia ipasavyo miundombinu ya majitaka, hususan katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea, ili kuepuka kuziba kwa mifumo hiyo na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Meneja Usimamizi wa Mifumo ya Majitaka wa DAWASA, Mhandisi Erick Mutalemwa, amesema matumizi yasiyo sahihi ya miundombinu hiyo yamekuwa chanzo kikubwa cha changamoto, hasa wakati wa mvua.
Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakielekeza maji ya mvua kwenye miundombinu ya majitaka, jambo linalosababisha mifumo hiyo kuzidiwa na kusababisha majitaka kutiririka mitaani.
“Pia kumekuwa na matukio ya wizi wa mifuniko ya chemba za majitaka, hali inayosababisha chemba hizo kubaki wazi na kuruhusu maji ya mvua pamoja na taka ngumu kuingia ndani ya mfumo huo,” amesema Mhandisi Mutalemwa.
Ameeleza kuwa DAWASA inaendelea kufanya kazi saa 24 kushughulikia changamoto za majitaka na kuwaomba wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona vitendo vya uharibifu au uhujumu wa miundombinu hiyo ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Kwa upande wake, mkazi wa Mikocheni, Lameck Singo, amesema changamoto nyingi za majitaka zinazowakumba wananchi zinachangiwa na matumizi mabaya ya miundombinu hiyo na baadhi ya wananchi.
“Niwaombe wananchi wenzangu tutambue kuwa suala hili linahusisha afya zetu. Tuepuke kuhujumu miundombinu hii ili kuzuia usumbufu wa mara kwa mara unaotokea pindi majitaka yanapoziba na kutiririka mitaani. Pia tuhakikishe tunajenga mifumo sahihi ya kupitisha maji ya mvua badala ya kuyaelekeza kwenye miundombinu ya majitaka,” amesema Singo.
