Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YATUA NA SULUHISHO LA MAJI SHARIF SHAMBA
21 Sep, 2026
DAWASA YATUA NA SULUHISHO LA MAJI SHARIF SHAMBA

Wakazi wa Mtaa wa Sharif Shamba, Kata ya Sharif Shamba, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, wameeleza kupata nafuu ya huduma ya maji baada ya kuanza kutumia maji kutoka kisima kinachoendeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).

Mhandisi wa Mkoa wa Kihuduma wa DAWASA, Aaron Chilo, amesema kisima hicho kina uwezo wa kuzalisha lita 10,590 za maji kwa saa, kiasi kinachowezesha kuhudumia wakazi wa Sharif Shamba na maeneo jirani.

Amesema DAWASA inaendelea kuwaunganisha kwenye mfumo wateja ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo, ili kuongeza idadi ya wakazi wanaonufaika na maji kutoka kwenye kisima hicho.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sharif Shamba, Athuman Dilunga, amesema kisima hicho kimekuwa mwarobaini wa changamoto ya maji katika eneo hilo, huku viongozi wa mtaa wakiendelea kushirikiana na DAWASA kulinda miundombinu.

“Kisima hiki kimekuwa mwarobaini wa changamoto ya maji katika mtaa wetu. Kwa sasa tunapata maji safi na salama muda wote. Baadhi ya wateja wameathiriwa na ujenzi wa barabara, lakini DAWASA inaendelea kuwaunganisha,” amesema Dilunga.

Mkazi wa eneo hilo, Mwanaisha Juma, ameipongeza DAWASA akisema upatikanaji wa maji umeondoa usumbufu uliokuwa ukiwakabili wakazi hapo awali.

“Kwa kweli tunaishukuru DAWASA kwa kutimiza dhamira ya Serikali ya kumtua mama ndoo kichwani. Zamani hatukupata maji ya uhakika, lakini sasa huduma imeboreshwa,” amesema.

DAWASA inaendelea kutekeleza miradi na kuboresha miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam  na Pwani kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo.