Wizara ya Maji

Dar es Salaam Water Supply And Sanitation Authority (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWAFIKIA WAKAZI ZAIDI 20,000 WALIOPO NJE YA MTANDAO
07 May, 2025
DAWASA YAWAFIKIA WAKAZI ZAIDI 20,000 WALIOPO NJE YA MTANDAO

Zaidi ya Wakazi 20,000 wa Wiaya ya Kigamboni, Kinondoni, Ubungo Temeke na Ilala wanatarajiwa kunufaika na huduma ya majisafi kupitia utekelezaji wa mradi wa majisafi unaoendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira a Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). 

Mradi huu ambao umeanza kutekelezwa katika Mwaka huu wa fedha 2024, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka ujao wa fedha 2025.  

Akieleza kuhusu utekelezaji wa mradi Msimamizi wa Mradi wa maji nje ya mtandao Mhandisi Azizi Namanga amesema kuwa utekelezaji wa mradi unahusisha ujenzi wa vizimba 50 vya kuchotea maji pamoja na ujenzi wa mtandao wa mabomba ya inchi 3 na inchi 1 ya kusambaza maji kwa wananchi kwa umbali wa kilomita 45.35. 

"Kwa sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 60, ambapo kazi kubwa iliyofanyika ni ulazaji wa mabomba ya ukubwa wa inchi 3 mpaka inchi 1 ya kusambaza maji kwenda kwenye vizimba vya maji," ameeleza Mhandisi Namanga. 

Ameongeza kuwa mradi utanufaisha mitaa mbalimbali ya Wilaya tajwa, ambapo kwa Wilaya ya Kigamboni, mitaa itakayonufaika ni pamoja na Buyuni, Kisarawe II, Mbutu na Kichangani. Kwa Wilaya ya Ubungo, mitaa itakayonufaika ni pamoja na kwa Unju na Ukombozi. Kwa Wilaya ya Temeke mradi utanufaisha mitaa ya Makuka Kaskazini, Kokoto, Kwa Zomboko, Mbagala, Kurasini Mji mpya. 

Kwa Wilaya ya Ilala mradi utanufaisha mitaa ya Gongo la Mboto, Rada - Majohe, Kipunguni B, Pugu Stesheni, Kajiungeni na Kisumo. Na kwa Wilaya ya Kinondoni mradi utanufaisha mitaa ya East Africa, Mazinde,  small garden na Mbezi Mtoni.

Naye mwenyekiti wa mtaa wa Buyuni ndugu. Shabani Omari ameeleza furaha yake kwa Mamlaka kwa namna ambavyo hawajasahaulika kwa kutafutiwa ufumbuzi wa wakazi wa maeneo ya mbali kupata huduma yq maji iliyo salama.

Kwa upande wake Brigita Mrisho mkazi wa Buyuni Kigamboni ameelezea furaha yake ya utekelezaji wa mradi huu na kusema jitihada hizi zinaleta matumaini ya kuwepo kwa maji ya uhakika na ya kutosha. 

"Tunaishukuru sana Serikali kupitia DAWASA kwa kuona umuhimu wa sisi wananchi kupatiwa huduma hii kwani tunapata maji kwa tabu kutoka kwenye visima ambavyo hatuna uhakika wa usalama wa maji hayo "ameeleza bi. Grigita.

Mradi huu unatekelezwa na DAWASA kwa gharama ya Shilingi milioni 738,899,494 kwa fedha za ndani.