Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWAFIKIA WANANCHI CHALINZE WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA
09 Oct, 2026
DAWASA YAWAFIKIA WANANCHI CHALINZE WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) imeweka dawati la huduma kwa Wateja katika Kata ya Pera, halmashauri ya Chalinze kwa lengo la kuwafikia wananchi na kutoa elimu kuhusu huduma za maji na majitaka.

Akizungumza katika dawati hilo, Afisa huduma kwa wateja mkoa wa kihuduma Chalinze Bi. Lilian Bosco amesema wananchi wamepewa elimu kuhusu usomaji sahihi wa mita za maji, ulipaji wa bili kwa wakati, utunzaji wa miundombinu ya maji pamoja na njia mbalimbali za kufanya malipo ya bili na kuomba huduma ya maji mtandaoni.

"Wananchi wameelimishwa kuhusu namna ya kuwasiliana na DAWASA pindi wanapokutana na changamoto za huduma pamoja na umuhimu wa kutumia Majisafi na salama kwa afya zao"amesema Bi Lilian. 

Naye Mwenyekiti wa Kata ya Pera, Ndugu Yusuph Mgweno, alitembelea dawati hilo na kueleza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya jitihada za DAWASA za kuimarisha huduma kwa wateja na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma za maji.