Wizara ya Maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA)

TIRA Logo
DAWASA YAWAFUATA WANANCHI WILAYA YA KINONDONI
29 Jun, 2026
DAWASA YAWAFUATA WANANCHI WILAYA YA KINONDONI

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefungua dawati la huduma kwa wateja katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za huduma ya maji zinazowakabili wananchi.

Akizungumza katika dawati hilo, Afisa Huduma kwa Wateja wa DAWASA, Ndugu Salama Hamidu amesema hatua hiyo inalenga kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama na ukusanyaji wa maoni kuhusu huduma zetu.

“Kupitia dawati hili, tunapokea kero za wananchi moja kwa moja, tunazifanyia kazi kwa haraka na kuzifuatilia hadi zipate ufumbuzi. Lengo letu ni kuhakikisha changamoto za maji katika Wilaya ya Kinondoni  zinatatuliwa kwa wakati,” amesema Ndugu Salama

Ndugu Benedict Siwi mkazi aa Magomeni amesema uwepo wa DAWASA leo katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni umeongeza matumaini ya kutatuliwa kwa changamoto za muda mrefu za maji.

“Awali tulikuwa tunapata ugumu mkubwa kufuata huduma za DAWASA, lakini leo nimepata urahisi kwa kufikisha malalamiko yangu na kupata majibu hapahapa. Naamini changamoto zetu zitapatiwa ufumbuzi,” amesema Siwi.

DAWASA inaahidi kuendelea kuboresha huduma zake kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na wananchi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika katika maeneo ya Wilaya ya Kinondoni.